Dk Mpango awataka viongozi dini, wananchi kuliombea taifa

DODOMA; MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amewataka viongozi wa dini, waumini na Watanzania kuliombea taifa kuwa na amani hususani katika kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Alisema ni muhimu kuliombea taifa kupata viongozi wenye hofu ya Mungu, waadilifu na wanaojali haki za wanyonge.

Akiambatana na mkewe, Mbonimpaye Mpango, wameungana na waumini mbalimbali katika Misa Takatifu ya Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Mwaka Mpya 2025 iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska, Kiwanja cha Ndege, Dodoma.

Advertisement

Alisema kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha taifa linakuwa na amani hivyo ni vema wakaliombea taifa.

Akizungumza na waumini mara baada ya misa hiyo, Makamu wa Rais ameungana na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali kuwatakia Watanzania wote heri na baraka kwa mwaka 2025.

Dk Mpango aliwahimiza waumini kuiombea dunia amani kutokana na machafuko yanayoendelea katika maeneo mbalimbali. Pia, alisisitiza kuwaombea Watanzania wenye matatizo mbalimbali waondokane na changamoto hizo.

Aliwasihi Watanzania kutumia vema mwaka 2025 hususani kipindi cha mvua kupanda miti, maua na kudumisha usafi katika maeneo yote ya nchi.

Misa Takatifu ya Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Mwaka Mpya 2025 imeongozwa na Padri Afrikanus Kimario.