Dk Mwigulu ataka ushirikiano wa kikanda mapambano dhidi ya saratani
WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema kuwa Afrika haiwezi kushinda vita dhidi ya saratani ikiwa kila nchi itafanya kazi peke yake.
Amesema kuwa ili kufikia malengo ya mapambano dhidi ya saratani, kunahitajika kuwepo kwa ushirikiano wa kikanda na wa bara zima katika utafiti, mafunzo, kubadilishana wataalamu na kubadilishana rasilimali, teknolojia pamoja na uzoefu.

Ametoa wito huo leo leo Februari 12, 2026 alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya miaka 30 ya Taasisi ya Saratani Ocean Road, yanayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Tanzania iko tayari kushirikiana na nchi zote za Afrika na kupitia Taasisi ya Saratani Ocean Road tutaendelea kuwa kituo cha ushirikiano wa kikanda na bara zima katika mapambano dhidi ya saratani,” amesema.

Dk Mwigulu amesema kuwa kupitia simulizi za machapisho ya kitafiti na sayansi ambazo wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road na Tanzania kwa ujumla wameyafanya, yamekuwa na mchango mkubwa ndani na nje ya nchi kisera na kiutendaji katika mapambano dhidi ya saratani.
Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu ameiagiza Wizara ya Afya kuandaa mkakati madhubuti wa kupunguza idadi ya wagonjwa wapya wa saratani ili kupunguza athari kwa rasilimaliwatu, uchumi na ustawi wa Taifa kwa ujumla.

“Kutokana na tahadhari ya wataalamu wa afya kutoka Shirika la Afya Duniani kuhusu ugonjwa wa saratani kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 ifikapo mwaka 2030, Wizara ya Afya mnapaswa kuandaa mikakati ya kupunguza idadi ya wagonjwa wapya,” amesisitiza.



