Dk Mwinyi ahimiza amani Dira 2050

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema mafanikio katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanategemea uwepo wa amani, uongozi bora na ukuaji mzuri wa uchumi.

Dk Mwinyi alisema hayo wakati wa uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 uliofanyika Dodoma katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC) jana.

Alisema Dira 2050 ni nyenzo muhimu inayotumiwa na taifa katika kufanikisha maelengo ya maendeleo ndani ya muda uliokusuduwa.

“Mafanikio ya utekelezaji wa dira ya maendeleo yanategemea sana mambo matatu; amani, uongozi bora na ukuaji wa kiuchumi,” alisema Dk Mwinyi.

Aliongeza: “Ni faraja kuona kuwa Tanzania ina vigezo hivyo kwa kuwa na amani, uongozi bora wa serikali yako (Rais Samia Suluhu Hassan) na mafanikio katika maendeleo ya uchumi tunayoyapata yanathibitisha Tanzania ina mwenendo mzuri wa ukuaji wa uchumi wake”.

Dk Mwinyi alisema dira hiyo itatoa muelekeo wa Tanzania, wapi inatarajia kufika katika miaka 25 ijayo katika kuimarisha ustawi wa wananchi.

Alisema nia ya serikali ni kuona dira hiyo inatekelezwa kwa mafanikio makubwa na aliwahimiza wananchi kuipokea dira hiyo kwa matumaini ya kuleta ustawi wa maisha katika mambo muhimu kwani imezingatia matakwa yao.

“Dira hii imezingatia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo kwa kila mtanzania na taifa kwa ujumla, hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuelewa wajibu wake katika kufanikisha utekelezaji mzuri.”

Alisema dira hiyo imezingatia matakwa na imewashirikisha wananchi katika mambo ya msingi ya kuandaa dira hiyo.

Alisema ushiriki wa makundi tofauti katika uandaaji wa dira hiyo kunafanya mchakato huo kuwa jumuishi.

“Ni ndoto, matarajio na matamanio ya watanzania yamezingatia kwa kiasi kikubwa katika hatua za maandalizi na watanzania walipata fursa kuchangia maoni yao.”

Aliipongeza timu ya walioshiriki kuandaa dira hiyo kuwa wamefanikiwa kuzingatia mambo ya msingi katika uandaaji.

Katika hatua nyingine Dk Mwinyi aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita katika kufanikisha utekelezaji wa mpango wa taifa wa maendeleo pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 inayomalizika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button