Dk Mwinyi ataka kasi PPP viwanja Sabasaba

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema sasa ni wakati wa kuwa na uwanja wa kisasa wa maonesho ya kimataifa ya biashara ya Dar es Salaam.

Dk Mwinyi alisema hayo wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam jana.

Aliipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kukamilisha mpango kazi na hatua ya ujenzi katika hatua iliyopita na akasema sasa ni wakati wa kuwa na uwanja bora.

“Katika hili, serikali imezingatia marekebisho ya sheria ya PPP ya mwaka 2023 kwa kuondoa urasimu wa michakato katika utekelezaji wa miradi kama hii yenye faida kwa nchi na wananchi, hivi sasa sheria si kikwazo tena cha miradi muhimu kama huu,” alisema Dk Mwinyi.

Aliongeza: “Natoa wito kwa Wizara ya Viwanda na Biashara na TanTrade pamoja na wadau muhimu kuhakikisha mpango huu unaenda kwa kasi na unaleta tija kwa pande zote.”

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis alisema mamlaka hiyo ipo katika mpango wa kuboresha miundombinu ya viwanja vya maonesho ili kuongeza hadhi na kuwa kitovu kikuu cha biashara Afrika.

Latifa alisema TanTrade itatekeleza mpango huo kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC).

“Tunashirikiana na kituo cha PPP kupitia usimamizi wa Mkurugenzi Mtendaji, David Kafulila ambaye ametupatia ushauri na tunaendelea kufanya kazi naye na wataalamu ili kuweza kufanikisha mradi huu kwa ufanisi,” alisema Latifa.

Alisema idadi ya washiriki wa maonesho ya mwaka huu imeongezeka kwa asilimia 10.2 ikilinganishwa na mwaka jana.

Latifa alisema kuongezeka kwa washiriki kumechangiwa na uboreshwaji uliofanywa katika maeneo mbalimbali ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo yameongeza ufanisi.

“Ndiyo maana tunasema Sabasaba Kidijiti mifumo yetu imetuwezesha kufanya kazi kwa asilimia 99 hadi kufikia Julai 6, tulishughulikia asilimia 99 ya maombi ya nafasi, vitambulisho na uuzaji wa tiketi,” alisema.

Aliongeza: “Washiriki wengi ni mashuhuda kwamba vitambulisho mara hii vilikuwa si tatizo kubwa, unapakia taarifa zako na unapata kwa kupitia mifumo yetu ya ndani”.

Latifa alisema matumizi ya Tehama yameongeza uwajibikaji na uwazi katika kutekeleza majukumu ya mamlaka ikiwemo ugawaji wa nafasi kwa washiriki.

Akizungumzia kuhusu ongezeko la wanaotembelea maonesho, Latifa alisema hadi juzi, watu 290,583 walirekodiwa kuingia katika maonesho hayo ikilinganishwa na watu 128,959 waliotemebelea maonesho hayo kwa kipindi kama hicho mwaka jana.

“Jana (juzi) kwenye banda la Maliasili na Utalii tulirekodi watembeleaji zaidi ya 195,000 kati ya hao 54,454 walikuwa ni watoto,” alisema.

Wakati huo huo, alisema TanTrade imeendelea na Programu ya Sabasaba Urithi Wetu na kubainisha kuwa mwaka huu wanafunzi 90 wa shule za sekondari kutoka mikoa mitano ya Kigoma, Pwani, Mbeya, Unguja na Stone Town Zanzibar wameshiriki programu hiyo.

Alisema dhamira ya programu hiyo ni kuwaandaa vijana ambao watakuja kuendeleza dhima ya maonesho ya Sabasaba katika miaka ijayo.

“Pia walitembelea miradi mbalimbali ikiwemo bandari, reli ya kisasa (SGR) na viwanja vya ndege vya taifa. Programu hii ni muhimu kwa sababu tunataka watakaokuja kuturithi sisi waijue Sabasaba na waimarishe kama ambavyo sisi tunajaribu kufanya,” alisema Latifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button