RAIS wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ametoa wito kwa taasisi zinazotoa mafundisho ya Kurani zilenge pia kusomesha tafsiri yake kwani ufahamu wa aya zinazosomwa ni jambo zuri katika kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha na makatazo yake.
Aidha, amewahimiza wale wote wenye uwezo kutumia kipindi hiki cha Mwenzi Mtukufu wa Ramadhani na kutoa sadaka kwa watu wenye uhitaji wakiwemo yatima, wajane na watu wenye ulemavu ili nao wapate faraja. Rais Mwinyi aliyasema hayo Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye mashindano ya kimataifa ya kuhifadhi Kurani yaliyoandaliwa na Taasisi ya Al-Hikma.
Alisema katika kipindi cha Ramadhani na baada ya kipindi hicho Waislamu wote wamehimizwa kuisoma Kurani kwa kuwa kuna fadhila mbele ya Mwenyezi Mungu. Aliipongeza Taasisi ya Al-Hikma kwa kuandaa mashindano hayo ya kuhifadhi Kurani ambapo kwa miaka miwili aliyohudhuria mashindano hayo ameona kuna mabadiliko makubwa kwa vijana wengi kuweza kuhifadhi Kurani.
“Taasisi ya Al-Hikma inastahili pongezi kwa kazi kubwa ya kuanda mashindano haya ya kimataifa ambapo mwaka huu yanajumuisha washiriki 20 kutoka mataifa ya Afrika na watatu maalumu kutoka nje ya Afrika,” alisema.
Alisema ni wazi kuwa ni fursa nyingine ya kuitangaza Tanzania kimataifa kwa kuwa mashindano hayo yanaonekana dunia nzima na kuwawezesha watu walio sehemu mbalimbali duniani kuyafuatilia.
“Tujitahidi kusoma Kurani katika mwezi huu wa Ramadhani na baada na kuzingatia mafundisho yake ili kutekeleza ibada mbalimbali tunazozifanya kwa usahihi…jaya ni mashindayo ya pili nashuhudia kuona mwamko mkubwa wa kusoma Kurani,” alieleza.
Alisema jitihada za kuhifadhi Kurani zina manufaa kwani zinawandaa mashehe na waalimu watakaoisimamia vyema dini hiyo. Alihimiza watu wote wenye uwezo kutoa sadaka kwa watu wenye uhitaji wakiwemo yatima, wajane watu wenye ulemavu kwani ni vyema wakakumbukwa na kusaidiwa ili wapate faraja na wanaotoa kufaidika na fadhila za kutoa sadaka katika mwezi huu.
Kwa upande wake, Shehe Mkuu na Mufti wa Tanzania, Abubakar Zuberi Bin Ally, alisema tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo kumekuwa na mabadiliko makubwa nchini ambapo vijana wengi wamekimbilia kuhifadhi Kurani.
“Tumepewa kitabu cha Kurani, kilichokamilika kama hatuongoka kwa kitabu hiki au kufanikiwa tusitegmee kuongoka au kufanikiwa tena. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ametengeneza kitabu kimtengeneze mwanadamu,” alisisitiza. Alizitaka Madrasa zote nchini zianze kazi ya kuhifadhi Kurani na kurudi kufundisha watu kuhifadhi ili kuilinda na kufanikiwa duniani na akhera.