Dk Nchimbi ajivunia tija mbolea ya ruzuku nchini

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema ruzuku ya mbolea imekuwa chachu ya mageuzi ya kilimo cha mahindi mkoani Rukwa.

Mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema hayo kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Jimbo la Kalambo mkoani Rukwa.

Dk Nchimbi amesema uzalishaji umeongezeka kutoka tani 273,000 hadi 405,100 katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema katika kipindi hicho kiwango cha ruzuku ya mbolea kiliongezeka kutoka tani 3,565 hadi kufikia tani 10,392 na uzalishaji wa mbegu ukipanda kutoka tani 870 hadi 1,500.

Dk Nchimbi amesema hatua hiyo imesaidia wakulima kuongeza tija na mapato, hivyo kuimarisha uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla.

SOMA: Kampeni za Dk Nchimbi zilivyowasha moto wa ushindi Mwanza

Amesema katika eneo la umwagiliaji skimu mpya zitaundwa ili kupunguza utegemezi wa mvua, huku ekari 367 zikitengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.

Dk Nchimbi amesema serikali ya CCM imeimarisha usalama katika Ziwa Tanganyika kwa mara ya kwanza kupitia uboreshaji wa vitendea kazi na boti mpya mbili zimetolewa kwa ajili ya ukanda wa Kalambo.

Amesema hatua hiyo imemaliza kilio cha muda mrefu cha wananchi na viongozi waliowahi kuongoza eneo hilo kutokana na changamoto za usalama wa majini.

Dk Nchimbi amesema Hospitali ya Wilaya ya Kalambo imeboreshwa na kufikia kiwango cha kisasa zikiwemo huduma za X-ray na upasuaji wa dharura.

“Zahanati zimeongezeka kutoka 52 hadi 56 huku vituo vya afya vikifikia 47, hali iliyoimarisha upatikanaji wa huduma karibu na wananchi,” amesema.

Dk Nchimbi amesema sekta ya elimu Kalambo imepewa kipaumbele na kwamba shule za msingi zimeongezeka kutoka 98 hadi 197 na sekondari kutoka 19 hadi 24.

Aidha, amesema walimu wapya 225 wameajiriwa na kufanya idadi ya walimu kufikia 925 na pia serikali imekamilisha ujenzi wa Chuo cha Elimu na Ufundi Stadi (VETA) Matai.

Kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama, Dk Nchimbi amesema serikali imetumia Sh bilioni nane kuongeza huduma hiyo na kuongeza kiwango cha upatikanaji kutoka asilimia 46 hadi 60.

“Visima virefu zaidi ya sita vimejengwa na kuhudumia zaidi ya wananchi 29,000 katika vijiji vya Kalambo,” amesema.

Dk Nchimbi amesema Sh bilioni 37.3 zimetumika kuboresha barabara za lami na pia barabara za changarawe zimeongezeka kutoka kilometa 40 hadi 69.

Katika sekta ya nishati, amesema vijiji vyote 111 vya Kalambo vimeunganishwa na umeme na kituo cha kupoza umeme cha Kalambo kikitarajiwa kukamilika na mradi wa TAZA wenye uwezo wa kuzalisha kilovoti 4,000.

Dk Nchimbi amesema katika miaka mitano ijayo serikali imepanga kuanzisha kongani za viwanda vya kusindika samaki na maziwa.

Pia, amesema serikali ya CCM imepanga kujenga zahanati 16 na vituo vya afya vitano, ujenzi wa shule mpya tano za msingi, madarasa mapya 30, shule tisa za sekondari na madarasa mapya 50.

Kwenye sekta ya maji, vijiji 83 vitapatiwa mradi wa maji safi na salama ambapo upatikanaji wa huduma hiyo unatarajiwa kufikia asilimia 92.

Aidha, Dk Nchimbi amesema CCM imepanga kuimarisha uvuvi kwa kujenga mabwawa, vizimba zaidi ya 30 vya kufugia samaki na kuanzisha kituo cha kukuza viumbe wa majini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button