Kampeni za Dk Nchimbi zilivyowasha moto wa ushindi Mwanza
MOTO wa kisiasa umezidi kushika kasi mkoani Mwanza baada ya Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi kuingia kwa kishindo na kuanzisha kampeni zilizoacha gumzo kubwa miongoni mwa wananchi.
Ziara yake, ambayo imegusa wilaya kadhaa ikiwemo Magu, Kwimba, Nyamagana, Ilemela na Kisesa, imeonesha upepo wa ushindi unaoinufaisha CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Safari ya Dk Nchimbi ilianza kwa mapokezi makubwa jijini Mwanza katika Uwanja wa ndege wa Mwanza alipokelewa na umati mkubwa wa wananchi ukiwemo msafara uliongozwa na pikipiki ishara ya mapenzi kwa mgombeaa huyo na CCM.
Maelfu ya wananchi walijitokeza kumlaki huku wakibeba mabango na kuimba nyimbo za kumsifu Rais Samia Suluhu Hassan na CCM kwa ujumla. Mkutano huo uliashiria namna wananchi walivyo na hamasa kubwa ya kushiriki katika uchaguzi na pia ulithibitisha nguvu ya CCM katika ngome hiyo muhimu kisiasa.
Katika hotuba yake, Dk Nchimbi anaweka bayana kuwa wananchi wa Mwanza hawana shaka na chama hicho. “Wananchi wameniambia Rais Samia alale usingizi kwa sababu ushindi ni wa CCM,” asema huku akishangiliwa na mamia ya wananchi.
SOMA: Mfumo ufuatiliaji miradi kuanzishwa kudhibiti rushwa
Moja ya hoja zilizopokelewa kwa shangwe kubwa ni pale Dk Nchimbi alipofafanua namna chama hicho kilivyopata ushindi wa mapema kupitia nafasi za udiwani na ubunge katika mikoa ya Mwanza na Geita.
Kwa mujibu wa Nchimbi, zaidi ya kata 90 mkoani Mwanza na kata 91 mkoani Geita wagombea wa CCM
wamepita bila kupingwa, jambo aliloliita, “Ishara ya ushindi wa kishindo” katika uchaguzi mkuu.
“Dalili hizi si za kawaida, ni uthibitisho wa imani ya wananchi kwa chama chenye misingi ya kazi na utu. Wananchi hawataki maneno, wanataka matokeo na CCM imeonesha kwa vitendo kwamba inajali mahitaji yao,” alisisitiza.
Katika Wilaya ya Magu, Dk Nchimbi anashirikiana na mgombea ubunge, Boniventura Kiswaga anayewasilisha orodha ndefu ya miradi iliyotekelezwa chini ya Rais Samia, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa Hospitali ya Wilaya kwa zaidi ya Sh bilioni moja, ujenzi wa daraja jipya kwa Sh bilioni 48 na stendi ya mabasi ya kisasa kwa Sh bilioni 10.
Aidha, Kiswaga anaeleza kuwa tatizo la maji mjini Magu limebaki historia kutokana na miradi iliyotekelezwa, huku elimu ikipewa kipaumbele kupitia ujenzi wa chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na ongezeko kubwa la shule na madarasa.
Kauli yake ya “Leteni mafiga matatu – Rais, Mbunge na Diwani wa CCM, ili ugali uive vizuri” ilipokewa kwa shangwe kubwa, ikionesha mshikamano wa wananchi na chama hicho.
Mkutano wa kampeni uliofanyika Kisesa na Magu uligeuka kuwa kipimo cha uelewa wa wananchi kuhusu Ilani ya CCM 2025/2030.
Uchunguzi wa mwandishi wa makala haya unabaini kuwa, wananchi sasa wanaweza kueleza kwa ufasaha ahadi za siku 100 za mwanzo za serikali ijayo ya CCM, ikiwemo ajira mpya kwa walimu wa sayansi, bima ya afya kwa wote na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka MwanzaIsaka. Kwa haki ya utani Dk Nchimbi anasema, “Nimesusa kuendelea na hotuba yangu kwa sababu ninyi tayari mmeeleza yote kwa usahihi.”
Kauli hiyo iliibua vicheko na kushangiliwa kwa nguvu, ikiashiria mshikamano wa wananchi na chama chao. Ziara ya Dk Nchimbi ilipata sura ya kipekee katika Wilaya ya Kwimba anapoahidi kuwa, serikali ijayo ya CCM itaweka mfumo maalumu wa ufuatiliaji miradi ili kudhibiti mianya ya rushwa na ubadhirifu.
Anasisitiza kuwa miradi mingi imekuwa ikichelewa kukamilika kutokana na changamoto za usimamizi na kwamba, CCM imejipanga kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi. “Maendeleo ni kama jipu, yanahitaji kusimamiwa kwa ukaribu na uadilifu,” anasema, huku akiahidi miradi mipya ya zahanati, vituo vya afya na shule za sekondari.
Kampeni za CCM Mwanza pia zilipata msukumo wa kipekee baada ya kada wa chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa kuhutubia umati katika Viwanja vya Furahisha. Msigwa anasisitiza kuwa kila mafanikio ya maendeleo nchini kwa sasa yana sura ya Rais Samia.
“Uongozi si jambo la kubahatisha. Hakuna chama kingine chenye mpango wa kweli zaidi ya CCM. Mnachagua CCM, mnachagua maendeleo,” anasema.
Viongozi wa chama mkoani Mwanza, akiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Lushinge wanahitimisha kwa kutoa takwimu za miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni tano iliyotekelezwa mkoani humo, ikiwemo Daraja la Kigongo-Busisi na Meli ya MV Hapa Kazi Tu.
Wanasema miradi hiyo ni kielelezo cha CCM kuendelea kuwa chama kinachoaminika Kwa ujumla, ziara ya Dk Nchimbi Mwanza imethibitisha kuwa upepo wa kisiasa upo upande wa CCM. Moto wa ushindi uliowashwa katika
Viwanja vya Furahisha, Magu, Kisesa na Kwimba unatarajiwa kusambaa mikoa yote, ukielekea kuhitimishwa na ushindi wa kishindo Oktoba 29.



