Dk Nchimbi: Tulinde Misitu

MAKAMU wa Rais, Emmanuel Nchimbi amesema sekta ya misitu ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi, akibainisha kuwa sekta hiyo inachangia takribani asilimia 20 ya Pato la Taifa. Dk Nchimbi alitoa kauli hiyo wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani pamoja na kampeni ya kitaifa ya upandaji miti iliyofanyika katika Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.
Amesema sekta ya misitu inayojumuisha ufugaji wa nyuki, uhifadhi wa wanyamapori na mifumo ya ikolojia ina nafasi muhimu katika soko la uchumi na ustawi wa taifa. Kwa mujibu wa Dk Nchimbi, Tanzania ina takribani hekta milioni 48.1 za misitu, sawa na asilimia 55 ya eneo lote la nchi kavu.
Kati ya eneo hilo, hekta milioni 44.7 sawa na asilimia 93 ni misitu ya uoto wa miombo, huku hekta milioni 3.4 sawa na asilimia saba ikiwa ni misitu ya uwanda wa chini, milimani, mikoko pamoja na mashamba ya miti. SOMA: Misitu ikitazamwa upya itaongeza zaidi pato la taifa
Ameeleza kuwa misitu ina mchango mkubwa katika maisha ya binadamu na maendeleo ya uchumi kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo uhifadhi wa wanyamapori, ufugaji wa nyuki, utalii, kilimo na upatikanaji wa maji kwa matumizi ya majumbani, viwandani na mashambani.
Akizungumzia maadhimisho ya siku hiyo, Dk Nchimbi amesema yanatoa fursa ya kuelimisha na kuhamasisha Watanzania kupanda na kutunza miti kwa ajili ya kulinda rasilimali misitu.Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Misitu ni uchumi endelevu, tuhifadhi kwa maendeleo ya taifa.”
Amesema kaulimbiu hiyo inaendana na mipango ya maendeleo ya taifa ikiwemo Tanzania Development Vision 2050 inayolenga kuhakikisha rasilimali za misitu zinachangia katika maendeleo ya nchi. Hata hivyo, amebainisha kuwa pamoja na umuhimu wake, misitu bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo utegemezi mkubwa wa rasilimali za misitu kwa ajili ya kuni, mkaa na mbao.
Changamoto nyingine ni pamoja na mifugo kuingizwa kwenye hifadhi za misitu kutafuta malisho, uvamizi wa ardhi kwa ajili ya makazi, kilimo na uchimbaji madini pamoja na matukio ya moto ndani ya hifadhi za misitu.Amesema hali hiyo imesababisha uharibifu wa misitu nchini kufikia takribani hekta 469,400 kila mwaka, kiwango alichosema ni kikubwa na kinahitaji hatua za haraka kudhibitiwa.

Dk Nchimbi amesema serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa maendeleo inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kulinda misitu, ikiwemo kutenga na kuhifadhi maeneo ya misitu pamoja na kuhamasisha kampeni za upandaji miti.
Ametaja hatua nyingine kuwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025–2030, inayolenga kulinda rasilimali za ardhi, misitu, maji na viumbe hai kwa ajili ya ustawi wa wananchi na uchumi endelevu.
Aidha, amesema kampeni ya kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka katika halmashauri mbalimbali pamoja na kuanzishwa kwa Kampeni ya Tanzania ya Kijani ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Dk Nchimbi pia ameelezea kuwa mkoa wa Lindi Region una rasilimali nyingi za misitu ya asili na mashamba ya miti, huku wananchi wake wakijishughulisha zaidi na kilimo, ufugaji na shughuli nyingine za kiuchumi. Ameagiza viongozi na wananchi kuhakikisha misitu inalindwa na kutunzwa, huku vijiji vikihimizwa kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi.
Amesema tangu kuanza kwa kampeni ya upandaji miti mwaka 2023, jumla ya miti milioni 113.1 imepandwa katika maeneo mbalimbali nchini kupitia kampeni ya Januari 27 ya Kijani. Amesisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kuendelea kumuunga mkono Samia Suluhu Hassan kwa kushiriki kikamilifu katika kupanda na kutunza miti ili kulinda mazingira na kuimarisha uchumi wa taifa.



