Dk Samia amefanya maajabu Tanga

TANGA: Mgombea Ubunge wa Jimbo la Tanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassimu Mbaraka, amesema kuwa Rais na Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, ameufungua Mkoa wa Tanga kwa kutekeleza miradi mikubwa ambayo ilikuwa ikisuasua kwa muda mrefu.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Mbaraka ameeleza kuwa Dk. Samia amefanikisha mambo makubwa ambayo hayajawahi kufanyika tangu nchi ipate uhuru.

“Kwanza kuna suala la bandari hili lilikuwa kilio cha muda mrefu cha watu wa Tanga lakini Mama umefanya uwekezaji wa takriban Sh bilioni 429. 1 hali ambayo imesababisha ufanisi wa utendaji kazi wa bandari yetu na kusababisha meli kuongezeka kutoka 118 kwa mwaka 2019/2020 hadi meli 457 kwa mwaka 2024/2025 ni mama amefanya haya ni mambo makubwa sana hayajawahi kufanywa na mtu yeyote yule” amesema Mbaraka.

Aidha, ameeleza kuwa kupitia uwekezaji huo mkubwa katika bandari, fursa za ajira zimeongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Kutokana na uwekezaji huo ajira rasmi zimeongezeka kutoka 217 hadi kufikia ajira 457, pia vibarua wameongezeka kutoka 6630 hadi 17871 haya ni mambo makubwa yaliyofanyika” amesema Mbaraka

Katika hatua nyingine, Mbaraka ametumia fursa hiyo kumuomba Dk. Samia kuhakikisha barabara ya Tanga–Segera inapanuliwa ili kupunguza msongamano na kuongeza ufanisi wa usafirishaji.
Aidha, Mbaraka amehimiza kukamilishwa kwa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, akisema hatua hizo zitazidi kuufungua Mkoa wa Tanga na kuufanya kuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji.

Mbaraka alihitimisha kwa kusema kuwa wananchi wa Tanga wana sababu zaidi ya milioni moja za kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba mwaka huu na kumpigia kura Dk. Samia ili apate ushindi wa kishindo, kwa kuwa ameandika historia kubwa ya maendeleo katika mkoa huo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button