Dk Samia amwaga sera Ngerengere

MOROGORO: MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kutoa shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu 8,320 ili kuwawezesha kuongeza mitaji na kujikwamua kiuchumi.
Ahadi hiyo imetolewa leo, Agosti 29, 2025, wakati Dk. Samia akihutubia mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu katika Kijiji cha Ngerengere, mkoani Morogoro, ambapo pia aligusia Barabara ya Bigwa–Mvuha–Kisaki inayounganisha maeneo mbalimbali ya eneo hilo.
Akizungumza mbele ya wananchi wa kijiji hicho, Dk. Samia amesema kuwa, pamoja na maendeleo yaliyopatikana chini ya uongozi wake, bado kuna changamoto zinazoikabili mkoa huo, hususan ukosefu wa miradi ya maji ya kutosha.

Amesema hali hiyo imesababishwa na uharibifu wa mazingira, ikiwemo ukataji wa miti ovyo, hivyo, ameahidi kuwa katika miaka mitano ijayo, serikali yake italipa kipaumbele suala hilo na kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwa wakati, huku akiwataka wananchi kuacha kukata miti kiholela na kutunza mazingira kwa ujumla.
Kuhusu miundombinu, Dk. Samia amegusia barabara ya Bigwa–Mvuha–Kisaki inayounganisha maeneo mbalimbali na makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya na kueleza kuwa barabara hiyo imekuwa ikisisitizwa na Mbunge wa Morogoro Vijijini, Hamis Taletale, itakamilika ndani ya miaka mitano ijayo.
Katika sekta ya afya, Dk. Samia amesema serikali itajenga vituo viwili vipya vya afya, zahanati saba, pamoja na kukamilisha ujenzi wa zahanati nne ambazo ujenzi wake bado unaendelea. Pia, amesisitiza kuwa serikali itahamasisha jamii kujiunga na huduma za bima ya afya kwa ajili ya ustawi wa afya ya wananchi.
Vilevile, ameahidi kujenga maghala mapya matatu kwa ajili ya kuhifadhi mazao na kuendeleza uzalishaji wa miche ya mazao ya mikarafuu, michikichi, mikorosho na mikokoa kwa ajili ya kukuza kilimo na kuongeza tija kwa wakulima.



