Dk Samia atekeleza ahadi, Tarsila apokea Mil 20/-

DAR ES SALAAM: BINTI aliyebuni na kutengeneza ndege nyuki (drone), Tarsila Mellita, amepokea Sh milioni 20 kutoka kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, fedha zilizowasilishwa na Msaidizi wa Rais Maendeleo ya Jamii, Jacqueline Kawishe.

Fedha hizo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais Dk Samia wakati wa kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane 2026 yaliyofanyika jijini Dodoma, baada ya kukagua banda la vijana aliloshiriki Tarsila wakati wa maonesho hayo.

Tarsila amebuni ndege nyuki inayotumika kusambaza viuatilifu kwenye mashamba, ubunifu unaolenga kuongeza ufanisi katika shughuli za kilimo kupitia matumizi ya teknolojia.
Binti huyo na vijana wenzake wanamiliki kampuni ya Nyika Ventures, ambayo itatumia fedha hizo kuendeleza na kuboresha teknolojia ya drone inayotengenezwa nchini.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuongeza matumizi ya teknolojia katika kilimo na kuwawezesha vijana kutumia ubunifu kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na kuongeza ufanisi katika uzalishaji.
–



