Dk Tulia afagilia maonesho Wizara ya Ujenzi

DODOMA; SPIKA wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson, amepongeza maonesho ya sekta ya ujenzi ambayo yanalenga kutoa elimu na huduma kuhusu kazi zinazofanywa na Wizara ya Ujenzi na taasisi zake.

Maonesho hayo yanafanyika kwa siku mbili katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma kuanzia leo Mei 27, 2024 hadi Mei, 28 mwaka huu.

Akizungumza wakati akifungua rasmi maonesho hayo, Spika Tulia amesema amefurahishwa na maelezo aliyoyapata katika mabanda mbalimbali kwenye maonesho hayo, ikiwa ni pamoja na kuelezwa kuwa kuna vifaa vya kisasa vya kupima barabara baada ya ujenzi kukamilika.

Amesema uwepo huo wa vifaa vya kisasa umempa matumaini makubwa, kwamba sasa barabara ikimaliza kujengwa, watu wa wizara hawatakubali kupokea barabara bila kujiridhisha na ubora wa ujenzi kwa kuipima.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza wakati wa kumkaribisha Spika Tulia, amesema katika maonesho hayo wabunge na wananchi watapata fursa ya kujifunza na kuzifahamu kwa ufasaha kazi zinazofanywa na taasisi zote zilizopo chini ya Wizara ya Ujenzi.

Habari Zifananazo

Back to top button