Dk Tulia: Fanyeni kazi, acheni majungu

Dk Tulia Ackson

SPIKA wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson amewataka wananchi kuacha tabia za kuendekeza majungu na badala yake wajikite katika kujenga Taifa.

Dk Tulia aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Mjini kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 kwa wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Tughimbe.

Alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu wasiopenda maendeleo wanapoona viongozi wakiwemo wa kitaifa wakifanya kazi nzuri kwa jamii wao wanapambana kutengeneza majungu na kukosoa utendaji ili kuleta mkanganyiko usio na faida kwa jamii.

Advertisement

Aliwataka wananchi wakiwemo wa jimbo hilo kuendelea kumuunga mkono katika majukumu yake ili aweze kuwatimizia mahitaji yao ikiwemo uboreshaji wa miundombinu, elimu, afya na mengineyo kwa kushirikiana na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na viongozi wa CCM na serikali akiwemo Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi na Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Humphrey Nsomba.

Viongozi hao walimpongeza Dk Tulia kwa namna ambavyo ameweza kufanya mabadiliko ya maendeleo ya haraka katika jimbo hilo kwa kipindi chake kifupi cha uongozi.

2 comments

Comments are closed.