Dk Tulia: Suala la umri wa binti kuolewa linafanyiwa kazi
DSM: SPIKA wa Bunge Dk Tulia Ackson amesema suala la sheria ya umri wa binti kuolewa linafanyiwa kazi na anaamini litafikia pazuri baada ya jamii kuwa na sauti moja.
Akizungumza wakati wa kuadhimisha siku ya mtoto wa kike amesema mabadiliko ya sheria ya ndoa wakati mwingine watu wanakuwa hawatuelewi kwani linachukua muda mrefu.
Amesema anakubaliana na mabadiliko ya sheria ya ndoa huku akitaja kuwa umri wa miaka 18 bado ni mdogo kwake.
“Lakini muelewe tu kuwa linafanyiwa kazi na ni mjadala mpana kwasababu lina mambo mengi ikiwa ni pamoja na mila na desturi zetu lakini pia Tanzania haina dini ila watu wake wana dini.”amesema
Amebainisha kuwa jamii zinamsukuma binti kuolewa akiwa amevunja ungo hivyo inahitaji kwenda pamoja ili wasije kumwacha mtu nyuma.
“Na kwa upande wa elimu wamepiga hatua ambapo binti akiwa yupo shule haruhusiwi kuolewa lakini mpaka anamaliza kidato cha sita sio rahisi kuwa na umri wa miaka 18 suala hilo linafanyiwa kazi na tunaamini itafika pazuri tutakubaliana na kuwa na sauti moja wakati utakapofika,”amesisitiza