Dodoma yapata bil 529/- miundombinu uchukuzi

BODI ya Wakurugenzi wakuu wa Benki ya Dunia imeidhinisha Dola za Marekani milioni 200 sawa na Sh bilioni 528.57 za Tanzania kwa ajili ya Mradi Endelevu wa Uchukuzi Dodoma (DIST).
Taarifa ya benki hiyo imeeleza mradi huo unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 430,000 wakiwemo wanawake 222,000 na vijana 81,700.
Imeeleza kuwa uwekezaji huo wa Benki ya Dunia utaboresha uchukuzi makao makuu ya serikali Dodoma, utaibua fursa za kiuchumi na kutengeneza ajira mpya 10,000 hadi ifikapo mwaka 2030.
Benki hiyo imeeleza uwekezaji huo utaboresha usafiri mjini katika baadhi ya maeneo na kuweka miundombinu ya maeneo ya watembea kwa miguu na mengineyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mradi huo pia utanufaisha madereva 750 wa vyombo vya usafiri wa umma na wengineo, utaboresha hali ya maisha na kuwa na mifumo stahimilivu na yenye ufanisi ya usafirishaji Dodoma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Nathan Belete alisema ukuaji wa Dodoma tangu mwaka 2016 unaleta fursa na changamoto.
Mradi wa DIST unajumuisha mambo matatu ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu na huduma za usafirishaji jijini Dodoma.
Benki ya Dunia imeeleza mradi huo pia utahusu uwekezaji ili kuwezesha wananchi kufika jijini kwa urahisi kwa kuboresha barabara za jirani ziwezeshe watumiaji wapya wa vyambo vya usafiri.
DIST pia itaanzisha mfumo wa uratibu kwa kuunganisha juhudi za wadau ikiwemo Wakala ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Jiji la Dodoma (CCD) na wengineo.
Mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano wa Tanroads, CCD, Latra na Tarura.



