DON ni filamu ya mwaka 1978 iliyojaa taharuki, ikiwa imeongozwa na Chandra Barot. Katika filamu hii, Amitabh Bachchan amecheza nafasi mbili; Don, bosi wa genge la kihalifu na Vijay, mkazi wa ‘uswazi’ mwenye maisha ya kawaida.
Vijay anafanana na Don, jambo linalomfanya ofisa wa polisi, DSP D’Silva (Iftekhar) kumshawishi, Vijay ajifanye ndiye Don, ili kupata taarifa na chanzo cha genge la uhalifu na kuziwasilisha polisi.
Don ni mhalifu aliyekubuhu. Licha ya kuwa kwenye orodha ya ‘Wanaosakwa Zaidi’ na Interpol, Don bado hashikiki kirahisi.
Mbali na polisi, Don anajitengenezea maadui wengine wachache, anamuua mmoja wa watu wake, Ramesh anapotaka kuachana na uhalifu.
Hii inamwongezea, Don maadui wawili wapya; Kamini (Helen), mchumba wa Ramesh na Roma (Zeenat Aman), dada wa Ramesh.
Kamini anamghilibu, Don ili kumkamatisha kwa polisi, mpango wake unashindwa kwa kuwa, Don anawazidi ujanja na kutoroka. Katika mchakato huo, Kamini anauawa.
Roma mwenye kisasi, ananyoa nywele zake, anajifundisha judo na karate, kisha anaingia katika kundi la Don baada ya kuwaghilibu akiwaaminisha kuwa yeye pia, ni mhalifu.
Don anavutiwa na ujuzi wake wa kupigana na kumruhusu afanye naye kazi bila kushuku chochote.
Baada ya majaribio mengi ya kumkamata, Don kushindwa, hatimaye polisi wanafanikiwa. Kwa bahati mbaya, Don anakufa, DSP D’Silva anapanga kulifikia kundi lote la uhalifu.
DSP anauzika mwili wa Don, akihakikisha watu hawajui kama Don amekufa; watu pekee wanaojua kuhusu kifo cha Don ni DSP, kuhani wa makaburi na wafuasi wake.
DSP anamkumbuka, Vijay anayepambana na maisha ya uswazi jijini Bombay, anamtaka kuwasaidia watoto wadogo wawili, ambao wanafanana sana na Don. Kisha DSP anampanga Vijay awe Don ili alimalize kundi lote.
Vijay ‘anarudi’ katika kundi la Don kama Don akijifanya amepoteza kumbukumbu (amnesia), Jasjit (Pran), aliyetolewa jela, anaanza kazi ya kulipiza kisasi dhidi ya DSP na kuwatafuta watoto wake, Deepu na Muni, ambao waliokolewa na kutunzwa na Vijay.
Vijay anafanikiwa kuiba shajara nyekundu na kuweka nyingine ya bandia na anawaambia kundi lake anakwenda kulipiza kisasi kwa DSP, lakini ukweli anakwenda kumpa shajara.
Roma anamfuata, Vijay anapona katika shambulizi na anamwelezea, Roma kwamba yeye si Don, bali Vijay. Roma hamwamini lakini DSP anaingilia na kumhakikishia.
Roma anamwomba, Vijay msamaha, na kujiunga naye. Vijay anakabidhi shajara kwa DSP, anaisoma na kugundua kwamba bosi mkuu wa uhalifu anaitwa Vardhan, lakini anashindwa kujua Vardhan ni nani.
Vijay anagundua mengi zaidi juu ya Don kupitia shajara na msaada wa Roma, anawatangazia kundi lake kuwa kumbukumbu zake zimerejea.
Wanasherehekea, lakini mambo yanageuka pale polisi wanapovamia sherehe, wakitumia taarifa za Vijay, lakini DSP anapigwa risasi, na Vijay anakamatwa kwa sababu polisi hawajui kama yeye si Don.
Vijay anawaomba polisi wampeleke kwa DSP, ambaye yupo hospitali. Vijay anamtaka DSP kuwaambia polisi yeye ni Vijay. Bahati mbaya DSP anakufa kutokana na majeraha na Vijay anahukumiwa.
Hata hivyo, anawatoroka polisi wakati akipelekwa kwenye jela yenye ulinzi mkali. Anaanza kujipigania mwenyewe akijaribu kuthibitisha kuwa hana hatia. Roma anakubali kufanya chochote anachoweza kumsaidia.
Anachanganyikiwa kwa kuwa polisi hawataki kuamini kwamba yeye ni Vijay, wakati huohuo kundi lake la uhalifu wanatambua kuwa yeye si Don.
Shajara ambayo, Vijay alimpa DSP – tumaini la mwisho la Vijay kuthibitisha hana hatia – inaibwa na Jasjit katika jaribio la kutafuta watoto wake waliopotea.
Vijay anawatoroka polisi na kundi la uhalifu kwa msaada wa Roma akijitahidi kuthibitisha kuwa hana hatia.
Katika mchakato huo, anagundua kuwa ofisa wa Interpol, R. K. Malik ndiye Vardhan, bosi halisi wa kundi la uhalifu, aliyemuua DSP, na pia amemkamata R. K. Malik halisi na kuchukua nafasi yake.
Baada ya Vijay kupigana dhidi ya watu wa Vardhan, Roma anaipata shajara. Mmoja wa wahalifu anampora na kuichoma moto.
Hapo ndipo mchezo unanoga, Vijay anapaswa kuthibitisha kwa polisi kuwa yeye si Don na kugeuza mashitaka kwa Vardhan.
Na hapa ndipo unaweza kujikuta ukiita maji ‘mma!’
0755 666964 au bjhiluka@yahoo.com