DRC: ICRC yaanza kuhamisha wanajeshi waliokwama Goma

GOMA : KAMATI ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imeanza rasmi zoezi la kuhamisha mamia ya wanajeshi na polisi wa DRC waliokwama kwa miezi kadhaa katika vituo vya Umoja wa Mataifa mjini Goma, baada ya mji huo kutekwa na waasi wa M23.

Kwa mujibu wa taarifa ya ICRC, misafara kadhaa ya magari imeondoka kutoka Goma kuelekea mji mkuu wa Kinshasa ikiwa na maafisa waliokuwa wametengwa katika vituo hivyo, pamoja na familia zao, huku wakiwa wameondolewa silaha zao kwa mujibu wa taratibu za kiusalama.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya mazungumzo marefu baina ya wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, Serikali ya DRC na kundi la waasi wa M23, ambayo yalilenga kuhakikisha uhamisho huo unafanyika kwa amani na bila madhara kwa walioko kwenye vituo hivyo.

Taarifa kutoka kwa maafisa wa usalama wa DRC na Umoja wa Mataifa zinaeleza kuwa kulikuwa na takriban wanajeshi 1,500 waliokuwa kwenye vituo vya UN hadi mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, wakisubiri hatua za kuwaondoa kwa usalama wao.

ICRC imesema zoezi hilo litafanyika kwa awamu kadhaa na litachukua muda wa siku kadhaa kukamilika, huku pande zote zinazohusika  za serikali, UN na waasi M23  zikiwa zimeahidi kushirikiana kuhakikisha usalama wa misafara hiyo unalindwa kwa hali ya juu.

SOMA: Wafanyakazi MSF wauwawa DRC

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button