‘Drones’ kudhibiti wahalifu misitu ya hifadhi

KILIMANJARO: WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),unaendelea na utaratibu wa kutumia mifumo ya teknolojia za kisasa zikiwemo za ndege zisizo na rubani (drones),kwa ajili kulinda misitu hatua ambayo inayosaidia ufanisi wa ulinzi na doria.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACC) ,James Nshare alisema hayo mjini Same alipoelezea mkakati wa uendelezaji uhifadhi misitu, utalii ikolojia na mafanikio ya Wakala katika kanda hiyo kwenye uchangiaji wa pato ya Taifa.
Nshare ambaye pia ni Kamanda wa Kanda ya Kaskazini inayojumisha mikoa ya Tanga, Kilimanjao na Arusha, amesema Wakala umehamia kulinda misitu yake kwa kutumia teknolojia mifumo ya kisasa ya urushaji wa ndege nyuki “ drones”.
“Lengo ni kutambua wahalifu wa maeneo ambayo hatuwezi kufika sisi kama watumishi ndani kabisa ya misitu na maeneo ambayo ni vigumu sana kuweza kupita kwa haraka na kwa muda mfupi” amesema Nshare
Amesema kwa kutumia teknolojia hiyo ya kisasa katika kutambua maeneo hayo , itawasaidia kuweza kudhibiti uhalifu na kulinda misitu .
“ Taasisi inajikita kwa matumizi ya sayansi na teknolojia kama inavyotakiwa kwa kutumia ndege nyuki (drone) ili kubaini uvamizi ndani ya misitu ya hifadhi katika kuhakikisha misitu inakuwa salama “ amesema Nshare.
Nshare amesema pamoja na matumizi hayo ya ndege nyuki kwenye doria pia Wakala unaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa misitu na kudhibiti mioto kwa kushirikiana na wadau wengine wa serikali.
Kuhusu sekta ya utalii Kamishna Msaidizi Mwandamizi Nshare amesema kuwa katika kaanda hiyo zaidi ya watalii 40,500 walitembelea katika vituo zaidi ya 15 vilivyopo kanda hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025.
Kutokana na jitihada hizo, Kanda hiyo imeongeza juhudi za ukisanyaji wa mapato ya serikali kutoka Sh bilioni nane hadi kufikia bilioni 14.
Nshare amesema, pia Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa Sh bilioni 1.2 kwa Wakala huo Kanda ya Kaskazini kwa ajili ya kuendeleza uwekezaji wa vivutio vya utalii ikolojia katika fukwe wa Bahari ya Hindi mkoani Tanga .
“ Tunaendelea kuwekeza miundombinu kuhakikisha kwamba idadi ya watalii inaongezeka na mpaka sasa hivi tumeshirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kwamba tunakuwa naendeleza hivi vituo vya utalii ,tunazo fursa kubwa uwekezaji katika maeneo yetu” amesema Nshare.
Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa TFS na Msaizidi wa Kamanda wa Kanda hiyo upande Usimamizi wa Vizuia vya ukaguzi wa Mazao ya Misitu na Nyuki, Rashid Shekivunga amesema pamoja na kuimalishwa kwa miundombinu na kuongezeka kwa makusanyo ya mapato ya yamemchangiwana kulimalishwa usimamizi wenye vizuia vya mazao ya misitu na nyuki.



