Dunia yamlilia Papa Francis

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa waumini wa Kanisa Katoliki nchini na duniani kote kutokana na kifo cha Kiongozi Mkuu wa kanisa hilo, Papa Francis, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88.

Kupitia taarifa iliyotolewa na kusambazwa katika akaunti rasmi ya Rais Samia kwenye mtandao wa Instagram, kiongozi huyo alieleza masikitiko yake makubwa kutokana na kifo hicho, akimwelezea kama mwalimu na kiongozi aliyeishi kwa kuhimiza maendeleo, amani na ustawi wa jamii kwa kipindi chote cha miaka 12 aliyohudumu kama Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani.

“Nimesikitishwa na taarifa ya kifo cha Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis. Katika kipindi chote cha miaka 12 akiwa kiongozi wa kanisa hilo, ameishi kama mwalimu aliyefundisha na kuhimiza ustawi na maendeleo ya watu, pamoja na kudumisha amani,” alisema Rais Samia.

Alisema kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Tanzania, anatuma salamu za rambirambi kwa waumini wote wa Kanisa Katoliki na kumuombea Papa Francis apumzike kwa amani katika makazi ya milele.

Ikumbukwe kuwa Februari 2024 Rais Samia alizungumza na kiongozi huyo wakati wa ziara yake ya kihistoria mjini Vatican akiwa Rais wa kwanza kutoka Tanzania kutembelea Makao Makuu ya Kanisa Katoliki kwa zaidi ya miaka 15.

Mazungumzo yao yalilenga katika mchango wa Kanisa Katoliki Tanzania, hususani katika sekta za elimu, afya na maendeleo ya kijamii.

Tanzania inakadiriwa kuwa na zaidi ya waumini milioni 12 wa Kanisa Katoliki. Hii inaifanya kuwa moja ya nchi zenye idadi kubwa ya Wakatoliki Afrika.

Mbali na Rais Samia, viongozi wengine wa dunia waliotuma salamu za rambirambi ni pamoja na Rais wa Kenya, William Ruto, Rais wa Uswisi, Karin Keller-Sutter, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Mfalme Charles III wa Uingereza, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, pamoja na viongozi kutoka Argentina, Italia, India, Marekani, Urusi na Israel.

Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, alimkumbuka Papa Francis kama ‘rafiki wa kweli’ wa watu wa Palestina.

Kifo cha Papa Francis kilithibitishwa rasmi jana Jumatatu ya Pasaka kupitia taarifa za vyombo vya habari vya kimataifa, ambapo ilielezwa kuwa alifariki dunia katika makazi yake ya Casa Santa Marta, Vatican, majira ya saa 1:35 asubuhi kwa saa za Roma, baada ya kuugua nimonia kali.

Mwadhama Kelvin Kardinali Farrell wa Kanisa la Roma ndiye aliyetoa taarifa rasmi akisema, “Askofu wa Roma, Francis, amerejea katika nyumba ya Baba.”

Papa Francis, ambaye alizaliwa kwa jina la Jorge Mario Bergoglio mjini Buenos Aires, Argentina mwaka 1936, alichaguliwa kuwa Papa wa 266 Machi 2013.

Alikuwa Papa wa kwanza kutoka Bara la Amerika, Papa wa kwanza kutoka Shirika la Kijesuiti, na wa kwanza kutoka nje ya Ulaya kwa zaidi ya miaka 1,000.

Kwa kipindi cha uongozi wake, alijulikana kwa unyenyekevu, kujitoa kwa jamii, kuwatumikia masikini, kulinda mazingira, na kuhimiza upendo na amani duniani.

Taarifa kutoka Vatican zinaeleza Papa Francis alikuwa akisumbuliwa mara kwa mara na matatizo ya mfumo wa upumuaji, hali iliyosababisha kufuta baadhi ya ziara zake, zikiwemo zile za Umoja wa Falme za Kiarabu mwaka 2023.

Alilazwa katika Hospitali ya Agostino Gemelli, Februari 14, 2025 na hali yake ilizidi kuwa mbaya Februari 18, kabla ya kurejea nyumbani baada ya siku 38 hospitalini.

Askofu Mkuu Diego Ravell wa Vatican alieleza Papa Francis aliomba mazishi yake yawe ya kawaida.

Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Maggid Mjengwa alisema Papa Francis atakumbukwa kwa msimamo wake wa kupigania amani duniani, kukemea mauaji ya wanawake na watoto wa Palestina katika vita ya Gaza, pamoja na mageuzi makubwa ndani ya Kanisa Katoliki.

Alisema kiongozi huyo ni miongoni mwa viongozi wachache wa dini waliokemea vikali ukiukwaji wa haki za binadamu na alijitokeza kuwapatanisha viongozi wa Sudan Kusini, hatua iliyosaidia kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Alisisitiza kuwa Papa alikuwa kiongozi wa dini aliyeishi maisha ya kawaida, tofauti na matarajio ya wengi kuhusu viongozi wa juu wa kidini.

Naye, mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia, Masta Stambuli alisema Papa Francis alikuwa mpenda amani na alijitokeza mara kwa mara katika maeneo yenye migogoro kuwaonya viongozi dhidi ya kutumia dini kama chanzo cha vita au vurugu.

Katika muktadha wa kitaifa, Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, linalojumuisha mikoa ya Shinyanga na Simiyu, Liberatus Sangu, alieleza kwa masikitiko kifo cha Papa na kumkumbuka kama kiongozi aliyemwezesha kuwa msaidizi wake akiwa Roma.

Alisema Papa Francis alifurahishwa na kazi yake ya kueneza injili alipokuwa akihudumu Vatican.

“Natoa wito kwa waumini wote katika kipindi hiki cha maombolezo kuwa watulivu na kumuombea, kwani amerudi katika nyumba ya Baba katika kipindi cha Ufufuko wa Kristo,” alisema Askofu Sangu.

Baadhi ya waumini wa Kanisa Katoliki mkoani Shinyanga, akiwemo Anikazi Kumbemba na Juliana Mathew, walieleza namna walivyoguswa na msiba huo, huku wakimkumbuka kwa kumteua Askofu Sangu kuwa Askofu wa jimbo hilo mwaka 2015. Kwa sasa, Askofu huyo ametimiza miaka 10 ya utume katika jimbo hilo.

Kutokana na kifo hicho, makardinali watano wamekuwa wakitajwa kushika nafasi hiyo akiwemo kardinali kutoka Ghana, Peter Turkson, Christoph Schonborn, Pietro Parolin wa Italia, Luis Tagle wa Ufilipino na Peter Erdo wa Hungary.

Imeandikwa na Selemani Nzaro, Shakila Mtambo na Tatu Mwakabana.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button