EAC iungwe mkono usimamizi, utekelezaji wa sarafu ya pamoja

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imefanikiwa kusimamia vyema Itifaki ya Soko la Pamoja katika miaka 25 baada ya kuanzishwa tena mwaka 1999.

Kazi kubwa iliyopo mbele kuanzia mwaka 2025 ni kusimamia na kutekeleza sarafu ya pamoja ikiwa ndio itifaki inayofuata kabla ya kuhitimisha na Shirikisho la Kisiasa.

Endapo itifaki ya sarafu ya pamoja itaridhiwa na nchi zote wanachama, manufaa mengi yatapatikana ikiwa ni pamoja na biashara kufanyika bila kubadili sarafu mipakani.

Advertisement

Kwa mujibu wa Sekretarieti ya EAC, itifaki ya sarafu hiyo ya pamoja inatarajiwa kukamilika mwaka 2031 ikiwa nchi zote zitapitisha maazimio ya uundwaji wa sarafu hiyo.

Tunaamini kutokana na mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji wa itifaki ya soko la pamoja, vivyo hivyo utekelezaji
wa itifaki ya sarafu ya pamoja utatimia.

Kutokana na ushirikiano wa kiuchumi kuimarika zaidi katika EAC ambayo ndio jumuiya kongwe zaidi Afrika, inaelezwa kuwa hali hiyo inashajihishwa na usimamizi na utekelezaji mzuri wa Itifaki ya Soko la Pamoja miongoni mwa nchi wanachama.

Moja ya mafanikio makubwa ambayo kila mwananchi ndani ya jumuiya anaweza kujivunia waziwazi ni kupanuka kwa jumuiya kutoka nchi tatu mwaka 1999 hadi nchi nane mwaka 2024.

Mafanikio hayo yanaendelea kutafsiri maono ya waasisi wa jumuiya hiyo, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania, Mzee Jomo Kenyatta wa Kenya na Dk Milton Obote wa Uganda ambao walilenga kuunganisha Afrika kupitia jumuiya zake.

Pamoja na mafanikio hayo, viongozi wa nchi za EAC wamefanikiwa kutekeleza itifaki mbili kati ya nne ambazo ni Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja ikiwa bado Itifaki ya Sarafu Moja na Shirikisho la Kisiasa.

Mafanikio hayo yote ni katika kipindi hicho cha miaka 25 na maendeleo ya Sarafu ya Pamoja yanaenda vizuri kwa sababu taarifa ya Sekretarieti ya EAC chini ya Katibu Mkuu, Veronica Nduva ilisema hadi kufika 2031 itakuwa imekamilika.

Kutekelezwa kwa itifaki ya soko la pamoja na Umoja wa Forodha vimesaidia kuanzishwa miradi mikubwa ya kimkakati ndani ya EAC kama Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga na mradi wa barabara za EAC.

Kuna kazi kubwa imefanyika kusaidia nchi zenye changamoto ya machafuko kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sudan Kusini na Somalia ili kuleta amani ya kudumu kwa njia ya mazungumzo na ya kijeshi.

Tunaisihi Sekretarieti ya EAC na wakuu wa nchi kupitisha mapendekezo ya uundwaji wa sarafu ya pamoja kuwezesha wananchi kufanya biashara bila kulazimika kubadili fedha.