EAC iwalinde wanawake biashara za kuvuka mpaka

BAADHI ya wanawake wanategemea biashara za kuvuka mpaka kupata riziki za kuendesha familia zao ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Juhudi za wanawake kujikwamua na kipato duni zimewapeleka hadi katika biashara za kuvuka mpaka kutoka nchi moja mwanachama wa EAC kwenda nyingine.

Lakini juhudi zao hizi zinakwamishwa na mambo kadhaa yaliyopo na yanayoendelea katika nchi wanachama wa EAC katika sekta ya biashara na uwekezaji.

SOMA: Kongamano EAC-2022 kukutanisha wafanyabiashara vijana 2000

Miongoni mwa mambo yanayoibuka kama kikwazo kikubwa kwa harakati za wanawake katika kujitafutia mkate ni vikwazo vya kibiashara vya kikodi na kiforodha.

Hili ni jambo kubwa ambalo kama halitasawazishwa na nchi wanachama wa EAC kwa ushirikiano na Sekretarieti ya Afrika Mashariki, ni vigumu kwa kundi hilo muhimu katika jamii kufaidi fursa lukuki zinazotokana na EAC.

Katika kujaribu kukabiliana na vikwazo hivyo kwa mwanamke, EAC kwa kushirikiana na sekretarieti pamoja na wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), wametembelea Kituo cha mpakani cha Namanga kujua changamoto zinazowatafuna wajasiriamali wanawake katika harakati za kutafuta pesa.

Katika ziara hiyo, wafanyabiashara wanawake waliwakilishwa na viongozi kutoka pande zote mbili za Mpaka wa Namanga.

Viongozi hao walitoa wasiwasi wao kuhusu vikwazo vinavyoendelea katika biashara ya mipakani, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vivuli vya kujikinga na jua na kulinda watoto na bidhaa zao wakati wa mvua, changamoto za pasi za muda pamoja na ukosefu wa vifaa vya kuwahudumia wafanyabiashara wanawake walemavu mpakani.

Katika kulitafutia ufumbuzi wa haraka, wafanyabiashara wanawake waliomba EAC kuchunguza mbinu za kutoa vivuli katika maeneo ya mipakani ili kuwalinda na kuwasaidia wafanyabiashara.

Tunaunga mkono juhudi hizi za makusudi zinazofanywa na EAC kwa kushirikiana na sekretarieti yake kuleta ahueni kwa wafanyabiashara wanawake ndani ya jumuiya kwa sababu hiyo ndio njia pekee ya kuleta ustawi wa wanawake katika jamii.

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva alikaririwa na vyombo vya habari akisisitiza kuwa wanawake wanajumuisha sehemu kubwa ya biashara ya mipakani ndani ya EAC.

Kauli yake kuwa wanawake wanashajihisha biashara ya mpakani kwa asilimia 60 na kufanya kipato cha msingi kwa familia nyingi za EAC kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa kikanda ni dhahiri.

Tunaamini ziara hiyo itaweka msingi imara wa kuboresha biashara za wanawake na kuwa kichocheo cha kuondoa changamoto zinazowasibu wafanyabiashara wanawake ndani ya EAC.

Tunaamini ziara hiyo itakuwa chachu kufanya ziara nyingine katika vituo vya mpakani ili kuendelea kuyatafutia majibu matatizo yanayowasibu wafanyabiashara katika maeneo ya mpaka na kurudisha nyuma juhudi za kujenga uchumi wa EAC.

Ni ukweli kuwa ushirikiano wa kikanda unaleta umoja kwa kuwa watu wenye umoja wenye njia rahisi za kuvuka mipaka, zinazosaidia biashara ndogo na za kati na ushiriki wa wanaume na wanawake katika biashara.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button