Elimu inahitajika watumiaji huduma za maji, nishati

WATUMIAJI wengi wa huduma za nishati na maji nchini wamekuwa hawajui mahali sahihi kwa kupeleka malalamiko yao wanapokuwa hawaridhishwi na huduma hizo kutokana na kukosa elimu ya kutosha.

Wengi wamekuwa wakipeleka malalamiko yanayohusu sekta hizo kwa wenyeviti na watendaji wa kata ,wakuu wa wilaya, wabunge au polisi hali inayoonesha bado elimu kuhusu uwasilishaji wa malalamiko na utatuzi wake haijafikishwa vyema kwa watumiaji.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dk James Andalile alisema hayo mjini Morogoro kwenye hotuba yake ya kufungua mkutano wa siku tatu wa kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati za watumiaji za mikoa wa Baraza la Ushauri la Watumiaji huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC).

Hotuba ya mkurugenzi huyo ilisomwa kwa niaba yake na Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki, Musira Nyirabu.

Dk Andalile alisema bado kuna watumiaji wengi wa huduma hizo hawana uelewa wa kutosha kuhusu haki na wajibu wao, na hata wanapokuwa hawaridhishwi na huduma wengi wao huwa hawaelewi ni wapi pa kulalamika ama mfumo gani watumie kuwasilisha malalamiko yao.

“Bado kamati nyingi hazijaanza kufikisha huduma maeneo ya wilayani hivyo ninawaagiza EWURA CCC kuendelea kutafuta vyanzo zaidi ya fedha ili kuziwezesha kamati hizo kupanua wigo wake wa utoaji elimu hadi ngazi za wilaya.”alisema Dk Andalile.

Dk Andalile aliwataka watoa huduma za nishati na maji ikiwemo Mamlaka za maji na Shirika la Umeme (TANESCO) kote nchini pamoja na vituo vya mafuta kutoa ushirikiano wa dhati kwa baraza la EWURA CCC,na wajumbe wa kamati za mikoa ili kwa kushirikiana waweze kutatua changamoto za wananchi.

Alisema EWURA akiwa ni mdhibiti itaendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali ili majukumu ya kamati hizo na baraza la EWURA CCC yaweze kufikiwa kwa ufanisi.

“Wito wangu kwenu kuendelea kujizatiti kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza uelewa kuhusu haki na wajibu wao na kuweza kufanya maamuzi na matumizi sahihi na endelevu ya huduma za nishati na maji na kuchangia kuboresha huduma hizo”alisisitiza Dk Andalile.

Pamoja na hayo Dk Andalile aliwapongeza wajumbe wa kamati hiyo kwa kazi kubwa wanayofanya kwa kujitolea,kutetea watanzania katika maeneo wanakoishi ili watoa huduma za nishati na maji watoe huduma zao kwa ubora unaokubalika.

Naye Kaimu Katibu mtendaji wa EWURA CCC , Stellah Lupimo alisema wameendelea kuwasaidia watumiaji kuwasilisha ama kulalamika kwa niaba yao juu ya changamoto mbalimbali zinazohusu sekta hiyo.

Lupimo alisema hadi kufikia Januari mwaka jana ,jumla ya walalamikaji 15,131 walikuwa wamesaidiwa kuwasilisha malalamiko yao kwa watoa huduma na kwa Mdhibiti.

Alisema kati ya hayo 7,515, yalihusu sekta ya maji, 7,059 ni umeme, 396 mafuta na 161 gesi ya kupikia majumbani.

Lupimo alitaja mafanikio mengine ni pamoja na kufanya progamu 7,324 za uelimishaji na kuwafikia watu 895,126 na kutoa misaada ya kisheria kwa walalamikaji wakati wa kusikiliza mashauri yao na mikutano yam waka ya kamati.

Kwa upande wa changamoto wanayokutana nayo ni ya kifedha kutokana na utegemezi wa chanzo kimoja cha mapato na kushindwa kufungua ofisi kila mikoa ikiwa na kuajiri watumishi wa kutosha.

Changamoto nyingine ni uhaba wa vitendea kazi ingawa wameanza zoezi kubaini vyanzo tofauti vya kifedha kwaajili ya utekelezaji wa majukumu yake.

Habari Zifananazo

Back to top button