PWANI: WILAYA ya Mkuranga imetajwa kupiga hatua kubwa katika sekta ya elimu, ambapo idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 114 mwaka 2021 hadi 127 mwaka 2024.
Aidha, shule za sekondari zimeongezeka kutoka 25 hadi kufikia 53 katika kipindi hicho.
Hayo yameelezwa na Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, siku ya Jumanne, Desemba 31, 2024, wakati wa mkutano uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Mwandege, kata ya Mwandege wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo yamefanikishwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amepongezwa kwa jitihada zake za kuimarisha elimu na huduma za kijamii.
Amesema kuwa shule zote zilizoongezeka zimejengwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, akiweka mkazo kwenye dhamira ya serikali ya kuhakikisha watoto wa Mkuranga wanapata elimu bora karibu na makazi yao.
“Mwaka 2020 tulikuwa na shule za msingi 114, lakini sasa tuna shule 127. Kwa upande wa sekondari, tulikuwa na 25, lakini leo tunazo shule 53. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa iliyofanyika na tunaendelea kushirikiana katika kuimarisha elimu wilayani hapa,” amesema Ulega.
Pamoja na ongezeko la shule, Wilaya ya Mkuranga pia imefanikiwa kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja. Waziri Ulega amebainisha kuwa ndani ya mwaka mmoja wa 2024 pekee, madaraja ya vivuko 11 yamejengwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, hatua iliyosaidia kuondoa changamoto za usafiri na usafirishaji.
“Kila mahali kulikokuwa na mto, tumekamilisha ujenzi wa daraja. Changamoto kubwa za usafiri ambazo zilikuwa zinakwamisha shughuli za kiuchumi sasa zimetatuliwa, na wananchi wanaweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi,” amesema.
Aidha Ulega amempongeza Rais Samia kwa kuwa mstari wa mbele kuleta maendeleo wilayani Mkuranga, akieleza kuwa juhudi zake zimesaidia kuboresha maisha ya wananchi na kuinua uchumi wa eneo hilo.
Mwisho.