ZAIDI ya wanafunzi 1,500 wa shule za sekondari Mbalamaziwa, Ifunda, na Mtitu mkoani Iringa wamenufaika na mpango wa “Elimu Yangu, Kesho Yangu,” unaotekelezwa na mradi wa Ng’ara chini ya uratibu wa Tumaini Foundation.
Mpango huu unalenga kuwawezesha wanafunzi wa kike kupata maarifa na ujuzi wa kukabiliana na changamoto za kijinsia, afya ya uzazi, na mazingira magumu ya kimaisha, na hivyo kuwaimarisha kielimu, kijamii, na kiafya.
Meneja wa Mradi wa Ng’ara, Anne Mwalyosi, amesema mpango huu unawapatia wasichana stadi za maisha zinazowasaidia kujitambua, kuweka malengo ya maisha, na kujiandaa kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo, hasa katika kipindi cha balehe.
Alisema wasichana wanafundishwa kuwa na malengo thabiti na kujitambua kama nguzo ya maendeleo yao ya baadaye.
“Mpango huu umelenga kuwasaidia wasichana kuendelea na masomo licha ya changamoto za kiafya na kijamii wanazokutana nazo,” amesema Mwalyosi.
Alizungumzia pia umuhimu wa wazazi kuwasaidia watoto wao ipasavyo pamoja na kutingwa na majukumu mengine, hali hiyo inatawafanya wasichana wasilalamike kukosa msaada wa kifamilia.
Mkurugenzi wa Tumaini Foundation, Tumaini Msowoya, amesema mpango unatoa elimu ya mzunguko wa hedhi na jinsi ya kujilinda kiafya akisisitiza kipengele hicho ni muhimu katika maisha ya msichana, na ukosefu wa elimu na vifaa sahihi wakati wa hedhi huathiri uwezo wa wasichana kuhudhuria masomo.
Pia amesema, mradi unatoa taulo za kike, jambo linalosaidia kupunguza utoro shuleni na kuondoa aibu inayohusiana na hedhi.
“Hali ya kujiamini kwa wasichana itasaidia kuimarisha viwango vya ufaulu kwa sababu wanahudhuria vipindi bila kukosa,” amesema Msowoya.
Amesema mradi huo pia unalenga kupinga mila potofu na ubaguzi wa kijinsia unaowakabili wasichana.
Alisema kwa kupitia elimu ya haki za kijinsia, wasichana wanaweza kukabiliana na changamoto kama ndoana mimba za utotoni, na unyanyasaji wa kijinsia.
Maria Sanga, mmoja wa wanafunzi walionufaika, amesema kwa kupitia mradi huo wamepata uelewa zaidi wa haki zao za kisheria na kijamii, na sasa wanaweza kujisimamia kwa ujasiri.
Aidha Tumaini Foundation inasema kuwa mpango huo unalenga pia kuimarisha uongozi wa wasichana kwa kuwafanya mabalozi wa mabadiliko katika jamii zao.
Amesema wanafunzi waliofanikiwa wanatumika kueneza ujumbe wa elimu kwa wenzao, na hivyo kujenga kizazi cha viongozi wa kike wenye uwezo wa kufanya maamuzi bora kwa mustakabali wa maisha yao na jamii kwa ujumla.
“Hii inasaidia kujenga kizazi kipya cha viongozi wa kike wenye uwezo wa kufanya maamuzi bora kwa mustakabali wa maisha yao na jamii kwa ujumla,” amesema.