Enzi mpya ya sekta ya habari, uchaguzi na matumizi ya akili unde

KATIKA nchi yoyote duniani, vyombo vya habari vina mchango mkubwa kuleta maendeleo kutokana na kazi yake kubwa ya kuhabarisha, kuelimisha, kuhamaisha, kuburudisha na hata kukosoa.

Kwa sasa sekta ya habari inashuhudia mabadiliko yanayosababishwa na uvumbuzi na teknolojia inayokua kwa kasi, watumiaji kubadili vitu wanavyopenda kufuatilia na ushindani mkubwa wa kupata watumiaji wa maudhui yanayozalishwa katika vyombo hivyo.

Kutokana na mabadiliko hayo, vyombo vya habari vinalazimika kuhakikisha vinaendana na mabadiliko hayo ili kuifanya sekta hiyo iendane na wakati na kusudi la uwepo wa vyombo hivyo liendelee kutimilika.

Kwa kutambua mabadiliko hayo na umuhimu wa vyombo hivyo kutafuta njia za kuendana nayo, Agosti mwaka huu Shirika la Habari la Kimataifa la Sputnik linalomilikiwa na Serikali ya Urusi, liliandaa programu ya mafunzo yanayoitwa “SputnikPro Writting Skills” kwa waandishi wa habari kutoka nchi zaidi ya 18 duniani kote wakishirikiana na wadau wengine.

Waandishi wa Habari kutoka nchi mbalimbali wakishiriki mafunzo.

Aidha, mwandishi wa makala hii alikuwa mmoja kati ya waliohudhuria mafunzo hayo yaliyofanyika mjini Moscow nchini Urusi na kuungana na waandishi wengine mahiri kutoka India, Afrika Kusini, Algeria, Uturuki, Serbia, Bulgaria, Congo-Brazzaville, Uganda, Pakistan, Bangladesh, Bahrain, Palestina, Tunisia, Indonesia, Thailand, Mongolia na Vietnam na Nicaragua.

Akifungua programu hiyo Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Sputnik, Vasily Pushkov anasema kuwa wamekuwa wakifanya kazi hiyo na matunda yanaonekana kwa waandishi wa habari waliohudhuria programu hiyo na kwamba, wanapanga kuanzisha ushirikiano ya muda mrefu.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo wakiwa katika majadiliano wakati wa uwasilishwaji wa mada.

“Jambo muhimu ni kwamba, watumiaji wa maudhui wa kisasa wanaishi kwa kanuni ya “papo kwa papo” ambayo ni kanuni muhimu sana kwa vyombo vya habari,” anasema Pushkov.

Kutokana na muktadha uliopo nchini kwa sasa wa mchakato mzima wa uchaguzi unaoendelea, mafunzo haya yalikuja kwa wakati sahihi kwa kuwa mada zilizotolewa zimejenga uwezo kwa wanahabari kuripoti habari kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na kuendana na mabadiliko.

Moja kati ya mada ambayo maarifa yake yanahitajika zaidi wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu ni kuhusu habari za uongo na potofu na namna ya kukabiliana nazo.

Akiwasilisha mada hiyo, Naibu Mkurugenzi wa Sputnik News, Victoria Polikarpova anasema habari za uongo ni tishio katika utoaji wa habari.

Anasema wanaosambaza habari hizo huwa na nia ya kushusha mawazo ya wale wanaokinzana nao mitazamo.
Anasema sekta ya habari pia imekuwa ikiandamwa na janga la kusambaa kwa habari za uongo na potofu kutokana na mitandao ya kijamii kuwa na nguvu ya kuzisambaza haraka zaidi kuliko zile za kweli.

Polikarpova anasema kumekuwa na ulimbukeni hadi katika baadhi ya vyombo vya habari ambapo kuna wakati ambao habari zisizo na ukweli huchapishwa kwa sababu za kibiashara wahusika wakijali zaidi kupata wafuasi kuliko kujali maudhui wanayoyapeleka kama yataleta madhara.

“Aidha, zinaweza kuwa kwa sababu za siasa kushawishi wapiga kura na watunga sera kwa manufaa ya kisiasa na kwa nia ya wahusika kueneza propaganda zao wenyewe,” anasema.

Mwandishi waHabariLEO, Lidya Inda akikabidhiwa cheti na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa wa
Sputnik, Vasily Pushkov baada ya kumaliza mafunzo ya “SputnikPro Writting Skills”yaliyofanyika Moscow, Urusi hivi karibuni.

Kimsingi anasisitiza kuwa, habari zisizo kweli na potofu husababisha madhara kwa watumiaji na vyombo vya habari.

Hii ni kwa kuwa maudhui hayo huathiri hisia za watumiaji na kufanya vyombo vya habari kwenda sawa na namna mitandao ya kijamii inavyofanya kuendana na wanachotaka watu.

Anasema jambo hilo linakwenda kinyume na miongozo ya uandishi wa habari.Ili kuhakikisha vyombo vya habari haviingi katika mtego wa kuripoti habari za uongo, Polikarpova anasema ni muhimu kufikiri kwa makini na kutathmini usahihi wa habari kabla ya kuzichapisha au kuzitangaza.

“Fikiri mara mbili na ikiwa una shaka lolote, usichapishe habari hiyo, jenga tabia ya kuuliza watu wengine kama wataalamu kuhakikisha taarifa, tahmini uhalali wa chanzo, fuatilia kama kuna machapisho kuhusu unachoripoti na usichapishe taarifa yoyote ambayo ipo nje ya taaluma yako,” anasisitiza.

Aidha, matumizi ya akili unde katika uandishi wa habari kwa sasa duniani kote ni jambo lisilokwepeka, lakini nalo lina athari zake mbaya kama yasipodhibitiwa na kuhakikisha hayatumiki kinyume na miiko ya taaluma ya habari.
Katika mada yake kuhusu namna akili unde inavyobadilisha ufanyaji kazi wa sekta ya habari, Mkuu wa Miradi Maalum wa Sputnik News, Mikhail Konrad anasema akili unde si mbadala wa mwandishi wa habari.

Anasema programu nyingi za akili unde zinazosaidia kufanya upembuzi wa data na kuhakiki taarifa zinasaidia kuokoa muda na kuongeza ubunifu na si mbadala wa mwandishi wa habari.

Anasema programu hizo ambazo nyingine wanaendelea kuzijaribu katika vyumba vyao vya habari zinasaidia kuandaa habari kwa kukusanya taarifa kutoka sehemu mbalimbali, kupendekeza kichwa cha habari, kupendekeza habari inayofanana na anayoandika mwandishi pamoja na kupendekeza video au picha zinzohusiana na mada.
Kazi nyingine ni kuhariri video, kubadili sauti kuwa maandishi, kutafsiri taarifa katika lugha mbalimbali, kutengeneza hotuba, kutambua sura, kuweka maandishi kwenye video na kutengeneza picha au video.

Hata hivyo, zipo njia za kutambua kama video au picha si ya kweli na kwamba huenda imetengenezwa kwa kutumia akili unde.

Kuhusu njia hizo, Polikarpova (Naibu Mkurugenzi wa Sputnik News) anataja baadhi kuwa ni pamoja na mwili au uso kubadilika badilika, video kutoendana na sauti, mazingira yasiyo ya kawaida na mjongeo usio wa asili.

Mwandishi wa habari aliyehudhuria programu hiyo kutoka Tanzania wa gazeti la Zanzibar Mail, Riziki Abdalla anasema mafunzo hayo yamempa maarifa na ujuzi mpya utakaomsaidia kuboresha taaluma yake kuendana ufanyaji kazi wa kisasa katika vyumba vya habari.

Anasema mada kama za namna ya kutambua habari isiyo sahihi na jinsi ya kujua kama video au picha ni ya kutengenezwa kwa akili unde zitamsaidia zaidi wakati huu ambao anaripoti habari za uchaguzi.
Anassisitiza kuwa, katu hawezi kujitumbukiza katika mkumbo wa kuripoti kila kitu, bila kujiridhisha na ukweli au uhalisia wa taarifa husika.

Mwandishi Sanket Gawhalle kutoka India, anasema kupitia programu hiyo, amepata maarifa na ujuzi kuhusu matumizi sahihi ya akili unde katika kuandaa na kuhakiki taarifa. Anaongeza kuwa ni muhimu kuhakikisha waandishi wa habari wanaenda sambamba na mabadiliko na kwamba, aliyojifunza atayatekeleza katika utendaji kazi wake.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button