Epukeni ‘WiFi’ ya bure kulinda taarifa

JAMII imeshauriwa kujiepusha na matumizi ya mitandao ya intaneti ya bure ili kulinda taarifa zao binafsi dhidi ya wizi wa kimtandao na udukuzi wa vifaa vyao vya kielektroniki.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Innocent Mungy wakati wa mafunzo maalumu kwa maofisa ulinzi wa taarifa binafsi.
Mungy alisema licha ya kuwa na mvuto kwa watumiaji, mitandao ya bure ya ‘Wi-Fi’ ni hatarishi kwa kuwa mara nyingi hutumiwa na wadukuzi kuiba taarifa binafsi kutoka kwenye vifaa kama simu janja na kompyuta mpakato.
“Duniani hakuna kitu cha bure. Mimi binafsi nimeacha kutumia free Wi-Fi baada ya kugundua kuwa baadhi ya watu hutumia mbinu hiyo kudukua taarifa zangu binafsi kupitia vifaa ninavyotumia,” alisema Mungy.
Aliongeza kuwa wahalifu wa mtandaoni wamekuwa wakitumia mbinu hiyo kuingilia mawasiliano ya watu na kunasa taarifa nyeti kama nenosiri, taarifa za benki na nyaraka za kikazi.
Katika hatua nyingine, Mungy aliwakumbusha maofisa hao kuhakikisha wanazingatia matakwa ya kisheria ya kuweka ombi la ridhaa katika maeneo yenye kamera za uangalizi (CCTV) ndani ya ofisi zao.
“Ombi la Ridhaa ni matakwa ya kisheria chini ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44. Hivyo, kama ofisi yako inatumia CCTV, ni muhimu kuweka taarifa inayoeleza wazi kuwa mtu anayeingia anakubaliana na uchukuaji wa taarifa zake, ikiwemo picha za video,” alisema.
Alibainisha kuwa lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha watu wanakuwa na ufahamu na kutoa ridhaa kabla ya taarifa zao kuchukuliwa au kuhifadhiwa kwa njia ya kidijiti, hasa katika maeneo ya kazi au biashara.



