fanyeni udaktari sio kukusanya mapato – Mnyeti

MAAFISA mifugo nchini wametakiwa kufanya kazi za udaktari wa mifugo waliosomea na kuwatembelea wafugaji badala ya kuwa wakusanya mapato wa halmashauri.

Taarifa ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti iliyotolewa leo Januari 25, 2024 akizindua Baraza la Veterinari Tanzania awamu ya sita baada ya baraza hilo kupata wajumbe amesema baadhi ya maafisa mifugo wamekuwa wakijikita zaidi kwenye kukusanya mapato ya halmashauri na minadani badala ya kuwatembelea wafugaji ili kujua matatizo yao.

“Maafisa mifugo kwenye halmashauri wanajifanya watumishi wa halmashauri kwa ajili ya kukusanya mapato kwenye minada kukusanya ushuru wa ng’ombe badala ya kufanya kazi za udaktari na kuwatembelea wafugaji,” Amesema Mnyeti

Aidha, amelitaka Baraza la Veterinari Tanzania kuhakikisha linachukua hatua zaidi kwa maafisa mifugo ambao wamekuwa wakifanya kazi kinyume na maadili pamoja na kuwapatia semina mara kwa mara ili kuwakumbusha wajibu wao kwa wananchi.

Amesema pia ifike wakati maafisa mifugo ambao wanakiuka maadili wafukuzwe kazi pamoja na kufutiwa leseni zao ili kazi hiyo ifanywe na watu ambao watafuata taratibu na maadili ya kazi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifuo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema ana imani maafisa mifugo ambao walikuwa wakituma maombi kwa ajili ya kusajiliwa kwenye Baraza la Veterinari Tanzania sasa wataanza kusajiliwa rasmi kwa kuwa baraza hilo tayari limezinduliwa.

Amefafanua kuwa amekuwa akipata ujumbe kwa njia ya simu kutoka kwa baadhi ya maafisa mifugo ambao wamekuwa wakihitaji kusajiliwa lakini hawakuweza kusajiliwa kwa kuwa baraza halikuwa na wajumbe.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari Tanzania Prof. Lughano Kusiluka amesema baraza limekuwa likisimamia sheria za veterinari kwa kuhakikisha wataalamu wanaohusika na kutoa huduma za afya za wanyama wafugwao na wasiofugwa wanafanya kazi kwa kufuata sheria na maadili.

Ameongeza kuwa kazi kubwa ya baraza ni kuwaandikisha na kuwaingiza kwenye daftari la baraza hilo na kufuatilia kiwango na huduma wanazotoa, kusimamia elimu ya wanyama inayotolewa na taasisi mbalimbali na kufuatilia kwa ukaribu wadau wapate huduma inayotakiwa.

Baraza la Veterinari Tanzania awamu ya sita lililozinduliwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti litadumu kwa miaka mitatu.

Habari Zifananazo

Back to top button