MOROGORO: MKAZI wa Kijiji cha Malulu wilayani Kilosa mkoani Morogoro, Festo Makambula ,35, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro akituhumiwa kumuua Mlinzi wa Kampuni ya Stigmaltin kwa kumchoma kisu kifuani na kusababisha kifo chake, huku chanzo kikidhaniwa kuwa ni mapenzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema mauaji hayo yametokea Februari 18, 2025 majira ya asubuhi katika eneo la Mululu Kisanga ambapo mtuhumiwa alimshambulia Rashid Kiupi ,49, ambaye ni shemeji yake wakati akielekea kazini na kumuua.
SOMA ZAIDI: ICC yaombwa kuchunguza mauaji ya waandishi
SACP Mkama amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi unaohusiana na mahusiano ya mapenzi kati ya marehemu na dada wa mtuhumiwa.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi kuhusu tukio hilo, huku akiwataka wananchi kuzuia vitendo vya uhalifu vinavyohatarisha usalama wa watu wengine.