Friends of Kagera waamua kugusa maisha ya wahitaji

KAGERA: Umoja wa wanachama wa mtandaoni wanaoishi ndani na nje ya Mkoa wa Kagera, unaofahamika kama Friends of Kagera, umeamua kuanza safari mpya ya kugusa maisha ya wahitaji na makundi maalumu katika jamii, ikiwemo wazee, watoto wenye mahitaji maalumu, wafungwa na wagonjwa kuanzia mwaka 2026.

Uamuzi huo umefikiwa katika mkutano wa sita wa umoja huo uliofanyika Bukoba, ambapo wanachama walikubaliana kuwa ni wakati wa umoja huo kurejesha shukrani kwa jamii inayowazunguka, kwa vitendo vya huruma na mshikamano.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Umoja huo, Mukhtari Sufiani, alisema tangu kuanzishwa kwa umoja huo miaka sita iliyopita, wamejikita zaidi katika kusaidiana wao kwa wao katika nyakati za furaha na changamoto, lakini sasa wameona umuhimu wa kupanua wigo na kuigusa jamii moja kwa moja.

“Tumekuwa tukisaidiana kama familia, lakini pia sisi ni sehemu ya jamii. Ndiyo maana tumeamua kuanza kutembelea familia za wahitaji, wazee, watoto yatima, magereza na hospitali ili kuleta faraja na matumaini kwa wale wanaohitaji msaada,” alisema Sufiani.

Wanachama wa umoja huo walieleza kuwa mpango huo wa kijamii utaimarisha umoja, mshikamano na mahusiano mema kati ya Friends of Kagera na jamii kwa ujumla, huku wakisisitiza kuwa kusaidiana ni msingi wa maendeleo ya jamii yoyote.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Mhandisi Johnston Mtasingwa, ambaye licha ya kutokuwa mwanachama wa umoja huo, alionesha kuvutiwa na jitihada za Friends of Kagera. Aliahidi kushirikiana nao katika shughuli za kijamii na kuunga mkono juhudi zinazolenga kuwafikia wahitaji.



