Geita waunda timu kukabiliana na mafuriko

MKUU wa Wilaya ya Geita, Hashimu Komba ameunda timu ya wataalamu itakayofanya ukaguzi na kutoa mapendekezo ya kukabiliana na mafuriko ya mvua za masika mjini Geita.

Komba amesema hayo akiwa kituo cha mabasi mjini Geita alipoambatana na Kamati ya Maafa ya Wilaya ili kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na mvua iliyonyesha Jumanne ya Novemba 05, 2024.

Advertisement

Komba amesema timu hiyo itaongozwa na Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Geita, maofisa wa mipango miji, na wahandisi kutoka Wakala wa Barabara Mjini na Vijiji (TARURA).

“Tunataka ndani ya kipindi cha siku 14 ufanyike ukaguzi wa eneo hili tunaposubiria stendi mpya, nini tunafanya ili adha iliyojitokeza isiweze kujirudia.

“Kazi ya pili ambayo tumewapa hii timu ni kuangalia njia za maji kwani yapo baadhi ya maeneo yalikuwa ni njia za maji, leo hii kuna wananchi wamejenga kwenye maeneo haya amesema Komba.

Amesema timu pia itapaswa kufanya ufuatiliaji wa kina juu ya mitaro inayopokea maji, njia zinazopitisha maji na maji yanapotokea ili kusimamia zoezi la usafi na upanuzi wa mitaro kuruhusu maji kupita.

Aidha Komba amewaka halmashauri kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi wa stendi mpya ili uweze kukamilika kwa wakati na kuruhusu stendi ya sasa ifanyiwe ukarabati kwa matumizi mengine.

Amewaomba pia wakazi wa Geita kuendelea kuwa wavumilivu kwani pesa za mradi wa stendi zipo tayari kupitia Pesa za Mradi wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTIC).

Komba amewataka wakazi wa halmashauri ya mji wa Geita kuzingatia usafi wa mazingira, ili njia zote za maji ziweze kuruhusu maji yaweze kupita, na maji yaweze kutiririka kwenda kwenye maeneo sahihi.

Mwenyekiti wa Stendi Kuu ya Mabasi mjini Geita, Khalid Hassan amesema kiini cha tatizo ni ufinyu wa mitaro na hivo ni vyema serikali ianze na upanuzi wa mitaro yenye uwezo wa kuhimiri mvua kubwa.