Geita yajipanga kuimarisha afya ya akili kwa watumishi

GEITA: SERIKALI mkoani Geita imeandaa mpango maalum wezeshi kwa watumishi wa umma kuwasaidia kuimarisha afya ya mwili na akili na kuwasaidia kuondokana na matatizo ya msongo wa mawazo kazini.
Katibu Tawala wa mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amesema hayo mjini Geita na kueleza mpango huo unahusisha ushirikishaji wa watumishi katika mashindano ya michezo ya kawaida na michezo ya asili.
Gombati ametoa taarifa hiyo wakati akifunga ‘Watumishi Bonaza’ awamu ya pili lililofanyika katika uwanja wa Nyankumbu mjini Geita na kueleza mpango huo pia unalenga kuimarisha umoja na ushiririkiano.
Amesema hatua hiyo inakuja kutokana na kukua kwa tatizo la magonjwa yasiyoambukiza hali inayochagizwa na mtindo wa maisha hali inayoashiria uhitaji wa mikakati ya ziada kukabili tatizo.

Katibu Tawala wa mkoa wa Geita, Mohamed Gombati akitoa zawadi kwa washiriki wa Watumishi Bonaza.
“Kupitia michezo tunaamini itatusaidia kujenga afya zetu na kukabiliana na magonjwa yasiyoambuza kama presha, kisukari, lakini vilevile kupambana na matatizo ya kisaikolojia.
“Tunaamini kwa ushiriki wa watumishi katika michezo hii tutawapa hamasa katika kutimiza majukumu yao ya kila siku, lakini vilevile tunatumia bonanza hili kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi”, amesema Gombati.
Gombati amesema wametoa maelekezo kwa taasisi zote kujiimarisha kwenye eneo la michezo, ili watumishi wapate fursa ya kushiriki michezo mbalimbali na wawe na mazoea ya kufanya mazoezi.
Ofisa Michezo mkoa wa Geita, Rodgers Bahati amesema mpango wa Watumishi Bonanza limefanyika kwa awamu ya pili ikiwa ni sehemu ya kutekeleza maagizo ya serikali kwa watumishi kufanya mazoezi.
Rodgers amesema ‘Watumishi Bonanza’ awamu ya pili lilishirikisha taasisi 20, kwa kuhusisha mashindano mbalimbali ikiwemo michezo ya jadi ili kuwajengea watumishi uzoefu tofauti nje ya maisha ya kazi.

Ofisa Michezo mkoa wa Geita, Rodgers Bahati
“Tukishatoka kwenye taasisi za umma sasa tunakwenda kushirikisha taasisi binafsi, kwa sababu Geita ni mkoa wa kimadini na kuna taasisi nyingi, tunataka tuwashirikishe tuwe kitu kimoja”, amesema Rodgers.



