GGML yafadhili kuimarisha usalama barabarani Geita
KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) imetoa ufadhili wa programu ya mafunzo ya usalama barabarani kwa maofisa usafirishaji 932 kitengo waendesha bajaji na pikipiki ili kupunguza ajali za barabarani wilayani Geita.
Programu hiyo imezinduliwa kwa kuhusisha mafunzo ya awamu ya kwanza kwa washiriki 491 ambao ni maofisa usafirishaji kutoka halmashauri ya manispaa ya Geita.
Mwakilishi wa Meneja Mwandamizi wa Mahusiano GGML, Elibariki Jambau amesema mbali na maofisa usafirishaji, elimu hiyo pia itafikishwa kwenye shule ambazo zitapatiwa mafunzo ya usalama barabarani.
SOMA: GGML yaendeleza mapambano dhidi ya rushwa Geita
Amesema Kauli mbiu ya programu hiyo ni “Uendeshaji Salama Barabarani Unaanza na Wewe” ambapo pia itaambatana na utoaji wa viaksi mwanga (reflectors) kwa waendesha bodaboda.
“Usalama barabarani siyo jukumu la serikali peke yake bali ni la kila mmoja, hii ni zaidi ya kampeni, ni jukumu letu kuchukua hatua kujifunza na kuongeza uelewa kwa changamoto inayotugusa wote.
“Kila ajali barabarani siyo hasara bali ni pigo kwa mstakabari wa Geita na Tanzania kwa ujumla. Hii ndio sababu kubwa ya GGML kushirikiana na halmashauri na jamii katika kutoa, amesema na kuongeza;
“Tunaamini kwa dhati kabisa kwamba uelewa, nidhamu na uwajibikaji barabarani unaweza kuokoa maisha ya watu, huu ni utamaduni tunaopaswa kuujenga pamoja na kuuishi,” amesema Jambau.

Mkuu wa Polisi wilaya ya Geita, Renatus Katembo amekiri kuwa program hiyo itaimarisha usalama barabarani kwani ni wazi kwamba waendesha bodaboda na bajaji wamekuwa chanzo kikubwa cha ajali.
“Hili kundi ni muhimu sana likapata elimu ya matumizi bora ya barabara, takwimu zinaonyesha kwamba bajaji na bodaboda wanapata sana ajali, inawezekana na kujisababishia au za kusababishwa,” amesema.

Katembo ametaja changamoto kubwa ya bajaji na bodaboda ni kuvunja sheria za barabarani kwa kusimama bila utaratibu, kuendesha vyombo kwa mwendo kasi pamoja na kubeba abiria zaidi ya uwezo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Bodaboda mkoa wa Geita, Fred Fidel ameishukuru GGML kwa program hiyo na kueleza kuwa ni njia sahihi kuwaongezea bodaboda uelewa ili wawe mabalozi wa usalama barabarani.

Fidel ameiomba GGML kupanua uwigo wa mafunzo hayo kwenye wilaya zote mkoani Geita ili kuwafikia waendesha bodaboda takribani 30,000 ndani ya mkoa huo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva Bajaji mkoa wa Geita, Mussa Kisoke ameiomba serikali kupitia Wakala wa Barabara Nchini(TANROADS) kuboresha alama za barabarani na maeneo ya maegesho ili kuweka mazingira rafiki kwa wasafirishaji.



