MAREKANI : KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameziomba nchi tajiri kutimiza ahadi zao ya kuzisaidia nchi masikini katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Hayo ameyasema wakati alipokuwa akitoa hotuba yake kwenye bunge la Lesotho, huku akisistiza kuwa ana matumaini kwamba hivi karibuni Afrika itapata viti vya kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Guterres yupo kwenye ziara ya siku tatu kusini mwa Afrika, na Jumatano aliitembelea Afrika Kusini. SAMA :Mamilioni ya dola kuhimili athari mabadiliko tabianchi
Wakati akiwa Lesotho nchi isiyo na bandari na inayopakana na Afrika Kusini, alitembelea bwawa la Katse ambalo ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuimarisha hifadhi ya maji.
Suala kuu ambalo Guterres ameangazia wakati wa ziara yake ni kuhusu fedha zinazohitajika kwa nchi masikini barani Afrika na kwingineko katika kukabiliana na ongezeko la joto duniani ambapo Bara la Afrika linachangia asilimia ndogo ya ongezeko la joto lakini ndio bara lililoathirika zaidi.
Hivi karibuni , mataifa mbalimbali yaliyokutana katika mkutano wa Azerbaijan walikubaliana kuchangia dola bilioni 300 kwa mwaka ili kuzisaidia nchi masikini kukabiliana na ongezeko la joto duniani.
Hatahivyo fedha hizo ambazo bado zimeonekana kuwa ndogo ukilinganisha na dola trilioni 1 ambazo mataifa yanayoendelea yalikuwa yanaitisha ili kukabiliana na janga hilo.
Guterres amesema mfuko mpya uliobuniwa kukadiria hasara na uharibifu kutokana na majanga ya asili yaliyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa kwenye nchi masikini lazima uanze kufanya kazi na kuchangiwa ipasavyo na wale wanaohusika kwenye uharibifu wa mazingira.
Chanzo: VOA