Habari matumizi ya nishati ya jua zaongezeka 79% Afrika Mashariki

DAR ES SALAAM: Ripoti mpya imebainisha ongezeko la asilimia 79 ya habari zinazohusu matumizi ya nishati ya jua katika kilimo Afrika Mashariki, kutoka habari 63 mwaka 2023 hadi 113 mwaka 2024.
Ripoti hiyo imeonesha magazeti kuongoza kwa utoaji wa habari hizo kwa asilimia 65.1, huku Tanzania ikishika nafasi ya tatu nyuma ya Kenya na Uganda kwa uzalishaji wa maudhui.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, alisema ongezeko hilo linatokana na mafunzo ya waandishi kuhusu nishati safi katika kilimo, yaliyofanyika mwaka 2023.
Balile amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kusukuma ajenda ya nishati safi kwa ajili ya kusaidia kilimo endelevu, hasa katika maeneo ya umwagiliaji na uhifadhi wa mazao.
Ripoti hiyo iliwasilishwa na Dk. Darius Mukiza wa ACME, akieleza kuwa waandishi 47 walipatiwa mafunzo kupitia vyombo sita kutoka Tanzania, Kenya na Uganda.
Kenya iliongoza kwa habari 43, ikifuatiwa na Uganda (36) na Tanzania (34). Hata hivyo, nyingi ya habari hizo hazikupewa nafasi za mbele katika magazeti na televisheni.
Uboreshaji katika matumizi ya vyanzo umeonekana, lakini ripoti imeeleza kuwa sauti za wanaume bado zinatawala kwa asilimia 74, huku teknolojia mpya zikikosa uwakilishi kabisa.
Ripoti inapendekeza mafunzo zaidi kwa waandishi na wahariri, pamoja na kukuza uandishi wa kina unaojumuisha data, wataalamu na uwakilishi wa kijinsia katika habari za nishati ya jua.