‘Hakuna mwanafunzi Dar atakayeshindwa kuanza shule’
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema hakuna mwanafunzi kuanzia shule ya awali, msingi wala sekondari jijini Dar atakayeshindwa kwenda shule kwa kigezo cha uhaba wa madarasa au madawati.
Makala ameyasema hayo leo Desemba 20, 2022 katika hafla ya utiaji saini, ambao umehusisha serikali kupitia Shirika la Reli (TRC) na Kampuni za ubia wa CCECC na CRCC kutoka China iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Kikwete – Ikulu jijini Dar es Salaam.
Amesema baada ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kutoa zaidi ya Sh Bilioni 12.3 za ujenzi wa madarasa, hakuna mtoto ambaye hatoenda shule.
“Mheshimiwa Rais, hali ya usalama ni shwari, nashukuru kwa Shilingi Bilioni 12.3 ulizotupa za kujenga madarasa 618, nikuhakikishie hakuna mtoto ambaye hatakwenda shule,” amesema.
Amesema ili kuhakikisha dhamira njema ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan inatimia, tayari ameelekeza watendaji wote kuhakikisha ajenda ya ukamilishaji wa madarasa inapewa kipaumbele, ili kabla ya mwezi Januari, madarasa yawe tayari na wanafunzi wasome.
Kwa mujibu wa Halmashauri ya Ilala makadirio ya wanafunzi watakaoanza masomo Januari mwakani kwa shule za awali ni 5,700, msingi 25,400 na kidato cha kwanza 30,500.
Aidha, Makala amesema Dar ndio Jiji la kibiashara, na ndio wanufaika wa kwanza wa mradi wa SGR.
“Hivi karibuni ulinipa fursa ya kwenda kujifunza mambo ya usafi Rwanda, wanakushukuru kwa kufungua biashara,” amesema na kuongeza:
“Unayoyafanya Mheshimiwa Rais yameandikwa kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, chama cha siasa kazi yake ni kushika dola, unayoyafanya unatekeleza kile kilichopo kwenye ilani,” amesema.