Halmashauri kutengua mikataba ya wazabuni wazembe

HALMASHAURI ya Wilaya ya Geita mkoani Geita imejipanga kutengua mikataba ya wazabuni waliopewa tenda ya kusambaza vifaa na madini ujenzi watakaobainika kushindwa kutekeleza wajibu wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Karia Rajabu ametoa kauli hiyo kufuatia ukaguzi wa timu ya menejimenti ya halmashauri kwenye miradi ya elimu yenye thamani ya Sh bilioni 1.8 iliyopo jimbo la Busanda.

Karia amesema baada ya kukagua miradi inayoendelea walibaini chanzo kikubwa cha miradi kutokamilika ndani ya muda ni wazabuni waliopewa tenda hawasambazi vifaa na madini ujenzi kwa wakati.

Advertisement

Ameongeza kuwa, menejimenti imebaini kiini cha changamoto ya wazabuni wa aina hiyo kwenye miradi ya umma inatokana na wazabuni hao kushinda tenda kwenye maeneo mengi ilihali hawana uwezo.

“Hizi ni kazi za halmashauri niwatake mnapotangaza tenda kwenye mfumo wa NEST muangalie uwezo wa wazabuni katika kukamilisha kazi wanazoziomba ili kuepuka hizi changamoto”, amesisitiza Karia

Aidha Karia amewataka walimu wanaosimamia ujenzi wa madarasa kuhakikisha vifaa vinavyotolewa na wazabuni hao vinakuwa na ubora unaostahili na wanapoona changamoto watoe taarifa kwa wakati.

Awali Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wa halmashauri, Rehema Mustafa ametaja baadhi ya miradi ambayo haijakamilika ni ujenzi wa shule ya amali iliyopo kata ya Nyamigota yenye thamani ya Sh milioni 584.

Amesema pia upanuzi wa miundombinu ya shule za kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Kagenge kwa thamani ya Sh milioni 481 na shule ya sekondari Lutozo kwa thamani ya Sh milioni 381.

Ametaja mradi mwingine ni mradi wa shule ya msingi mtaa wa Afya ambayo ilianza kwa nguvu za wananchi na baadaye kuendelezwa madarasa tisa kwa mfuko wa BOOST kwa thamani ya Sh milioni 351.

Deogratius Wilson ambaye ni miongoni mwa mafundi kwenye miradi iliyotembelewa amekiri kuwa wazabuni wanashindwa kusambaza madini ujenzi kwa wakati na ndio chanzo cha miradi kutokamilika.