Halmashauri ya Wilaya Geita kinara mashindano ya Umitashumta

GEITA: HALMASHAURI ya wilaya ya Geita imetangazwa kuwa mshindi wa jumla wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za msingi Tanzania (UMITASHUMITA) mwaka 2025 mkoani Geita.

Mashindano hayo yalifanyika mjini Geita kwa kuhusisha halmashauri zote za mkoa wa Geita kwa kuhusisha mchezo wa soka, mpira wa pete, mpira wa kikapu, mpira wa mikono, mpira wa wavu, riadha na fani za ndani.

Ofisa Michezo Mkoa wa Geita, Rodgers Bahati ametoa taarifa hiyo Juni mosi, 2025 katika hafla ya kufunga mashindano hayo yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya wasichana Nyankumbu, Manispaa ya Geita.

Amesema mashindano ya Umitashumita mkoani Geita mwaka 2025 yalihusisha wanafunzi washiriki 667 kati yao wavulana 336 na wasichana 331, walimu 69, waamuzi 20 na viongozi mbalimbali 26.

“Jumla ya wanamichezo 126 wamepatikana kuunda timu ya mkoa, pia kuna walimu 16 na daktari mmoja ambao watakaa kambini kwa siku tano kujiandaa na mashindano ya kitaifa Juni 07, 2025 mkoani Iringa”, amesema.

Ofisa Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Richard Magubiki amesema ushindi wa jumla umetokana na jinsi walivyofanya vizuri kwenye michezo yote iliyoshirikisha halmashauri sita za mkoa.

“Walimu wameonyesha utayari na kuweza kuwafundisha watoto namna ya kuweza kushirki na kufanya mazoezi katika viwanja mbalimbali ambapo kwa mwaka 2026 pia tumejipanga kufanya vizuri zaidi.

Magubiki amesema baada ya mashindano ya Umitashumita ngazi ya mkoa, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imetoa zaidi ya asilimia 75 ya wachezaji wanaounda timu ya Umitashumita ya mkoa wa Geita.

Ofisa Michezo Halmashauri ya wilaya ya Geita, Saguda Maduhu amesema wamefanikiwa kushinda vikombe zaidi ya 10 na kuwezesha wanafunzi 70 kuchaguliwa kwenye timu ya Umitashumita ya mkoa.

Katibu Tawala wa mkoa wa Geita, Mohamed Gombat ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Geita na kuagiza halmashauri zote ziweke mipango endelevu ya kukuza na kuendeleza michezo mashuleni.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button