Hati fungani ya Samia yanukia kwa wakandarasi

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa ameielekeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na taasisi za fedha nchini kuanzisha mchakato wa upatikanaji wa hati fungani ya miundombinu ya barabara (Tararua Infrastructure Bond).

Lengo la hati funguani hiyo ambayo itapewa jina la ‘Samia Bond’ ni kuwawezesha Makandarasi wa ndani mitaji.

Akizungumza katika kikao kazi na Menejimenti ya Tarura, Makatibu Tawala Wasaidizi Miundombinu, Makandarasi Wazawa, Wataalamu Washauri na Taasisi za Kibenki, kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Amesema anaamini hati fungani hiyo itasaidia kutatua changamoto za kifedha wanazokumbana nazo Makandarasi wa ndani na kuwawezesha kupata kazi za miradi mikubwa na waweze kuikamilisha kwa ufanisi.

“Matarajio yangu ni kuwa, hati fungani hii italeta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya miundombinu ya Barabara inayojengwa na TARURA na itaendana na kasi ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuwashirikisha na kufanya kazi na sekta binafsi, katika kutatua na kubuni mbinu za kuchochea gurudumu la kuwafikishia maendeleo wananchi,” amesema

Amesema, kwenye eneo muhimu la matengenezo ya barabara, fedha hupatikana kutokana na makusanyo ya kila mwezi hivyo matengenezo hutegemea kupatikana kwa fedha baada ya makusanyo.

“Hali hii wakati mwingine husababisha matengenezo kuchelewa tuangalie namna ya kupata fedha kwa wakati ili kuendeleza miundombinu yetu.

“Tafiti mbalimbali za Benki ya Dunia zinaonesha kwamba kuna madhara makubwa kiuchumi pale kazi za matengenezo ya barabara zinaposubiri au kuahirishwa na wameonesha kwamba ukiwekeza Dola Moja ya Kimarakeni kwenye matengenezo ya barabara zilizo katika hali nzuri sasa utaokoa Dola Nne hadi 10 za Kimarekani kulinganisha na iwapo matengenezo hayo yangeahirishwa.” Amesema Mchengerwa.

Habari Zifananazo

Back to top button