HEET kuboresha miundombinu ya elimu UDSM

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kinaendelea kutekeleza kwa mafanikio Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET), unaolenga kuboresha miundombinu, kuimarisha mitaala, na kukuza mfumo wa kujifunza kidijitali. Mradi huu ni kiungo muhimu katika kuhakikisha elimu ya juu inachangia uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu ya Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Oktoba 21, 2025, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu, Profesa William Anangisye, alisema HEET ni mpango wa kitaifa unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa ufadhili wa Dola za Marekani milioni 425. Profesa Anangisye alibainisha kuwa lengo kuu ni kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuhakikisha mitaala inalingana na mahitaji ya soko la ajira.

Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, UDSM imetengewa Dola milioni 49.5 (Shilingi Bilioni 121) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi kwa kipindi cha miaka mitano (Julai 2021 – Juni 2026). Mradi umejikita katika maeneo sita makuu, ikiwemo ujenzi wa madarasa, maabara, karakana na vituo vya kidijitali katika kampasi mpya za Lindi (Ngongo na Ruangwa) na Kagera. SOMA: UDSM wapokea vitabu msaada kwa wanafunzi

Kupitia HEET, UDSM imekamilisha ujenzi wa majengo mapya 11 ya kufundishia na ofisi za wahadhiri, hosteli za wanafunzi, kituo cha huduma za jinsia na mahitaji maalum, pamoja na kukarabati majengo ya Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia (CoET). Chuo pia kimeongeza kasi ya mtandao kutoka 1.5 Mbps hadi 10 Mbps, na vifaa vya kisasa vinavyowezesha wanafunzi zaidi ya 8,000 kujifunza kwa wakati mmoja. Zaidi ya masomo 1,000 sasa yanapatikana kupitia e-learning, yakiwemo ya wanafunzi 39,000 na wahadhiri 600.

Katika maboresho ya mitaala, UDSM imefanyia mapitio mitaala 250 ili yalingane na mahitaji ya soko la ajira, ikijumuisha muda wa mafunzo ya vitendo na ujuzi wa wahitimu. Watumishi 29 wamefadhiliwa kusoma Uzamivu na Umahiri katika vyuo vikuu vya kimataifa, ambapo asilimia 30 ni wanawake.

Kwa upande wake Naibu Mratibu wa HEET, Profesa Libelato Haule, alisema mradi umeongeza ubora wa elimu, upatikanaji kupitia e-learning, na ajira; zaidi ya asilimia 82 ya wahitimu hupata ajira ndani ya mwaka mmoja.

Utekelezaji wa HEET umeifanya UDSM kuwa kinara wa mageuzi ya elimu ya juu nchini, sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Mpango wa Tanzania ya Kidijitali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button