Samwel Swai :DAR ES SALAAM: KWA mara ya pili Chuo Kikuu cha Dr es Salaam (UDSM), kimepokea msaada wa vitabu 200 kutoka Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC), vitakavyoongeza maarifa kwa wanafunzi.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Maktaba chuoni hapo, Dk.Collins Kimaryo amesema hayo wakati wa hafla ya makabidhiano ya vitabu hivyo iliyofanyika chuoni hapo.
Dk. Kimaro amesema vitabu walivyopokea ni vya sanaa, historia, sayansi ma teknolojia.
” Vitabu vinagusa sanaa, historia, sayansi na teknolojia. Vinatufaa maana kazi za msingi ni kutoa huduma za machapisho mbalimbali.
” Vitabu tunavyopokea vitaongeza maarifa kwa wanafunzi, vitaongeza aina za majarida tuliyonayo, pia kuonyesha ushirikiano baina ya China na Tanzania, pia Chuo Kikuu na Kampuni hiyo,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo ya CCCC, Li Xuecai amesema wamekwenda kugawa vitabu chuoni hapo kwa mara ya pili matukio yanayoonyesha kwamba ni daraja la kuimarisha uhusiano kati ya China na Tanzania.
Amesema tukio hilo pia ni sehemu ya kubadilishana utamduni baina ya nchi hizo mbili.
“Nashukuru kufikia tukio la kugawa vitabu kwa mara ya pili, mwaka jana pia tuligawa vitabu katika maktaba hii,” amesema,
Kwa upande mwingine Mkurugenzi Mtanzania Taasisi ya Confucius, Profesa Aldin Mutembei ameishukuru kampuni hiyo kwa kutoa nakala hizo 200 chuoni hapo.
Amesema katika maktaba hiyo wanaendelea kujenga utamaduni baina ya Tanzania na China, pia kueleza watanzania namna gani China inaendelea.
Mutembei amesema katika maktaba hiyo kuna vitabu vinavyozungumzia utawala na mawazo ya China. Amesisitiza usomaji wa vitabu unasaidia kuchagiza afya.