‘Hekari 400,000 za misitu hupotea kila mwaka’ 

TAKRIBANI hekari 400,000 za misitu nchini zinatazamiwa kupotea kila mwaka kutokana na ukataji wa miti unaochochewa na shughuli mbalimbali za binadamu hususani matumizi ya kuni na mkaa.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Judith Kapinga alibainisha hayo jana katika hafla ya upandaji miti mkoani Geita iliyoratibiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Alisema tathmini hiyo imedhihirisha wazi kwamba matumizi ya mkaa na kuni ndio chanzo kikubwa cha ukataji miti na hivyo hatua za haraka zichukuliwe kukabiliana na tatizo kwa matumizi ya nishati mbadala.

“Hapa kwetu Tanzania kati ya hekari milioni moja ya miti inayokatwa, asilimia 70 ya miti hutumika kwa uzalishaji wa mkaa na hupelekea nchi yetu kuwa jangwa kwa asilimia 61.

“Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinasema takribani watu milioni nne hufariki kila mwaka kabla ya wakati kutokana na matumizi ya moto na nishati ngumu katika kupikia.”

Kapinga aliwapongeza Stamico kwa kuanza kuzalisha nishati mbadala ya kupikia (mkaa rafiki) kwani itasaidia siyo tu kupunguza athari za kimazingira lakini pia athari za kiafya kwa binadamu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Venance Mwasse alisema kukabiliana na athari za mazingira kwa kampeni ya msimu huu wa mvua Stamico wamejipanga kupanda takribani miti 10,000 nchi nzima.

Alisema walizindua kampeni kwa kupanda miti 2,000 mkoani Dodoma na kwa Mkoa wa Geita watapanda miti mingine 2,000 na wamejipanga kuitunza na kuisimamia iweze kukua.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Nchini (Femata), John Dinna alisema wameweka mwongozo kuhakikisha kila mgodi wa wachimbaji wadogo wanapanda miti kuwaunga mkono Stamico.

Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko alisisitiza Stamico kuwajibika kuwawezesha wachimbaji wadogo na kusimamia usalama wa mazingira ili kuendeleza sera ya uchimbaji salama bila uharibifu wa mazingira.

Habari Zifananazo

Back to top button