Heko Rais Samia, mcheza kwao hutunzwa

IKIWA imesalia wiki moja  kabla ya Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), jamii ya wanazuoni inaona umuhimu wa kumtunuku Udaktari wa Falsafa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM,  Dk. Samia Suluhu Hassan.

Unapozungumzia kutulia kwa siasa za Tanzania  katika zama hizi  jina la Dk Samia  halitaweza kuwekwa kapuni, litawekwa peupeni, litunzwe na kuenziwa na kila mpenda haki, demokrasia na umoja.

Kuzikwa kwa siasa za kushupaliana, vitisho, ubabe, kuimarisha sekta ya elimu, kuongeza nguvu ya bajeti katika sekta ya kilimo, kuimarisha uhusiano na mataifa ya nje ni miongoni mwa mambo makubwa  ambayo yanamuweka katika historia nzuri Rais Dk Samia.

Akiwa Rais wa Awamu ya Sita, Rais Dk Samia mara tu alipoingia Ikulu amehimiza na amekuwa muumini  juu ya kuheshimu haki za binadamu,uvumilivu wa kisiasa na kuhimiza siasa za kileo zenye kuzingatia hoja badala ya porojo, fujo na ubabe.

Katika kuthamini jitihada zake, falsafa zake katika ujenzi wa Tanzania mpya, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). kimeamua kumpa heshima kubwa na ya kipekee  kwa kumtunuku Shahada ya Udaktari  wa Falsafa.

Leo katika viunga vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam vilisheheni watu wa kila rika, kike , kiume.

Wananchi na jamii ya wanazuoni walifika kushuhudia tukio muhimu katika historia ya nchi yetu kwa kiongozi wetu kutunukiwa kiwango hicho cha elimu kwa kuthamini mchango wake kwa Umma.

Shahada ya Udaktari wa Uzamivu- PhD  ya heshima katika Falsafa  aliyotunukiwa  Dk Samia na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imebadili wasifu na kuandika historia mpya ya Rais Dk Samia  na wananchi wa Tanzania.

Kwa nini Chuo Kikuu  kimemtunuku Shahada ya Uzamivu katika Falsafa Rais Dk Samia?

Katika utaratibu wa  vyuo vikuu duniani, mtu anayetunukiwa shahada ya aina hii mara nyingi anakuwa ni mtu wa kipekee, mwenye sifa njema, muungwana, mchakapazi ambaye amefanya na anaendelea kufanya mambo makubwa na ya msingi katika jamii  na ambaye rekodi yake ya haki za binadamu inakuwa isiyoshaka na katika kuwatumikia raia wenzake.

Rais Dk. Samia anaingia katika rekodi ya utendaji bora na uliotukuka akionesha ushupavu wa uongozi, akionesha uwezo na uhodari sio tu katika kutawala uwanja wa siasa, bali hata katika uhusiano wetu na mataifa ya nje.

Ingawa wapo watakaosema haya na yale, lakini ukweli utabaki kuwa hivyo maana kila aliye na macho anaona umakini wake, utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM  ambayo imetafsiriwa katika mipango ya maendeleo ya serikali ni uthibitisho wa dhamira njema ya Rais Dk. Samia.

Malezi aliyopata Rais Dk. Samia kwa wazazi wake, ndani ya CCM katika jamii na serikalini yanamfunga kutokuwa kiongozi mbabe, Rais Dk. Samia  si kiongozi mwenye makeke, kama walivyo viongozi wengine katika mataifa mbalimbali tuliopata kuwaona au kuwasikia katika tawala zao.

Rais Dk. Samia si mtu mwenye visasi, chuki, si mtu wa kujilimbikizia mali, katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja  kama angekuwa kiongozi tamaa basi leo ungesikia miguno kutoka kwa wananchi kuwa “ahaa jumba lile la Samia, kiwanda kile cha mwanawe” licha ya kuwa pengine mwanawe anastahiki kuwa hivyo, lakini watu wasingefahamu hivyo.

Hakuna  hata chembe ya shaka kuwa Rais Dk. Samia na familia yake si katika viongozi wanaokumbatia mali, kwake yeye utumishi wa umma ni muhimu zaidi.

Kwa hakika ni Rais makini, mchapakazi na aliyetayari kujifunza kutoka kwa wengine, wawe wakubwa, wadogo na hata wafanyakazi wa kawaida, kwake yeye urais si kikwazo cha kuongeza weledi katika uongozi na katika siasa.

Umakini na umahiri katika kuongoza nchi ulianza kujitokeza katika siku 100 za mwanzo, namna anavyoshughulikia matatizo ya kijamii, anavyokerwa na tabia za ubabe na wizi wa mali za umma, anavyowajibika katika kusimamia utekelezaji wa maagizo yake, unatoa mwanga wa kule tuendako.

Maendeleo ya Tanzania  ndiyo kipaumbele chake,  imekuwa dira ya uongozi wake itakayompa muongozo wa kusimamia yale yaliyoainishwa kwenye Ilani na mwelekeo wa Sera za CCM wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Pengine isingelitosha kwa Rais Dk. Samia kuwa na mawazo chanya peke yake bila kuwa na nia ya kuyatimiza yale anayoyaamini.

Wataalam wa tasnia ya uongozi wanasema kwamba kuna wakati malengo yanakumbana na vikwazo, hivyo ni wajibu wa kiongozi  kusimamia uamuzi sahihi na kuwa mtu wa mwisho.

Rais Dk Samia si katika aina ya viongozi wanaofuata hisia zao, au vionjo vyake; hofu, woga, wasiwasi, hasira, chuki, kinyongo havina nafasi katika utawala wake.

Kwa mnasaba huo, tumeshuhudia hivi leo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, moja katika vyuo vyenye kuheshimika kimataifa na kikiwa miongoni mwa vyuo vyenye hadhi ya juu, kikimtunuku Shahada ya Udaktari wa Falsafa.

Heko Rais Dk Samia, mcheza kwao hutunzwa.

Habari Zifananazo

Back to top button