Hili la mawakili kwenda vijijini ni mwafaka

TANGU Machi mwaka jana, serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imekuwa ikiendesha Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambayo hadi sasa imekwishafika mikoa 18 nchini.

Kwa mujibu wa takwimu, mikoa ambayo imeshafikiwa na kampeni hiyo ni Dodoma, Manyara, Shinyanga, Songwe, Morogoro, Geita, Kilimanjaro, Njombe, Iringa, Katavi na Tabora.

Mikoa ya Mwanza, Lindi, Rukwa, Mbeya na Pwani itapata huduma hiyo kwa siku tisa kuanzia wiki hii. Kufikia Mei, mikoa yote pamoja na Zanzibar itafikiwa.

Takwimu pia zinaonesha kuwa watu zaidi ya 1,373,099 kutoka mikoa 18 wamehudumiwa na migogoro 11,244 iliwasilishwa na kati ya hiyo migogoro 2,791 ikiwamo iliyokuwa ya muda mrefu ilitatuliwa papo hapo.

Akihutubia juzi katika kampeni hiyo mkoani Lindi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameelekeza mawakili wa serikali
wapangiwe majukumu ya kutatua kero za wananchi kwa ngazi za kata na vijiji ili kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi hao ambao wanauhitaji.

Amemuagiza Mwanasheria Mkuu na wakuu wa idara zenye kero wafanye kazi usiku na mchana na kwamba kila taasisi inayohusika na utoaji haki ziwajibike kutoa haki hizo na wadau wa sekta ya sheria wajipange kuwafikia wananchi hadi vijijini.

Tunapongeza uamuzi huo wa serikali wa kuja na kampeni hii ambayo kwa mikoa hii 18 ambayo imefikiwa hadi sasa, imethibitisha kwamba kulikuwapo na uhitaji mkubwa kwa wananchi wa msaada wa kisheria.

Hivyo, hakuna ubishi kwamba uamuzi ulikuwa wa busara na kwa hakika unapaswa kuendelezwa hata baada ya kumalizika kwa mikoa yote kwani tunaamini bado kutakuwa na mahitaji zaidi kwa wananchi hawa.

Ndiyo maana tunaona kwamba agizo la Waziri Mkuu la kutaka mawakili wa serikali pamoja na wadau wengine wa sheria kufika katika ngazi ya kata na vijijini, ni la busara na litakuwa la maana kutokana na hali iliyojitokeza katika kampeni hivi sasa.

Kwa muda mrefu sasa, mawakili wengi wamekuwa wakifanyia kazi zao maeneo ya mijini na hivyo watu wa ngazi za chini, zikiwamo kata na vijiji kukosa huduma ya msaada wa kisheria, huku ikitambulika kwamba huko ngazi ya chini ndiko ambako pia kuna changamoto kubwa za masuala ya mirathi, ndoa, ardhi na mengineyo.

Uamuzi wa kuwataka mawakili wa serikali na wadau wa sheria kwenda kuwafikia wananchi hawa, unapaswa kutekelezwa bila kuchelewa kwa sababu tunaamini watasaidia katika kutatua changamoto tulizozitaja pamoja na nyingine zinazowakabili wananchi wa ngazi hizo.

Kunapopatikana haki, maana yake ni kwamba jamii inaishi kwa amani na utulivu. Kwa hiyo, kutatua changamoto hizo ni kuifanya jamii ya Watanzania iendelee kuishi kwa amani na kutumia muda wao mwingi katika uzalishaji mali badala ya kuhangaika kutafuta haki katika ama mahakama au mabaraza ya usuluhishi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button