Hongera EAC ukuaji mzuri wa biashara 2025

KATIKA gazeti la HabariLEO kuna habari kuhusu biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupanda hadi kufikia thamani ya Dola za Marekani bilioni 38.2 katika robo ya pili ya mwaka 2025.

Habari hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa juzi katika makao makuu ya EAC mkoani Arusha iliyoeleza mabadiliko makubwa katika biashara ya bidhaa za kimataifa katika kipindi hicho na kusisitiza uthabiti wa kanda kiuchumi na kuongezeka kwa ushindani katika masoko ya kimataifa.

Hili limetutia moyo sana kama wana Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na kuimarika kwa biashara ambapo imepanda kwa asilimia 28.4 ikiwa ni kutoka Dola bilioni 29.7 katika robo ya pili ya mwaka 2024 hadi Dola bilioni 38.2 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ufanisi mkubwa katika ukuaji huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na mauzo ya nje ambayo yalipanda kwa asilimia 40.5 ambayo ni sawa na Dola za Marekani bilioni 18.6.

SOMA: Mawaziri EAC kujadili utengamano uchumi, biashara

Tunazipongeza nchi zote nane za EAC kutokana na mchango wao mkubwa katika kufikia mafanikio haya muhimu yaliyogusa hadi katika uagizaji wa bidhaa za EAC kuongezeka kwa wastani wa asilimia 18.8 sawa na Dola bilioni 19.6.

Kutokana na matokeo hayo, nakisi ya biashara kwa kipindi hicho ilipungua kwa kiasi kikubwa kutoka Dola bilioni 3.2 hadi Dola bilioni 0.9, na hivyo kuashiria kuimarika kwa urari wa biashara ya nje.

Aidha, kwa upande wa biashara na nchi nyingine za Afrika iliongezeka kwa asilimia 42.9 sawa na Dola bilioni 9.3, ambayo sasa ni asilimia 24.5 ya jumla ya biashara.

Biashara ya ndani ya EAC ilikua kwa asilimia 24.5 sawa na Dola bilioni 4.6, ikiwa ni asilimia 12.1 ya jumla ya biashara.

EAC pia iliimarisha uhusiano wake wa kibiashara na masoko ya kanda za Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambayo yalichangia asilimia 9.9 na 15.2 kwenye biashara za kanda.

Mahitaji makubwa kutoka nje yanatoka nchi za China, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Afrika Kusini, Hong Kong na Singapore ambazo kwa pamoja zimechangia jumla ya asilimia 62.8 ya mauzo ya nje kutoka kutoka asilimia 40.1 mwaka 2024.

Tunafarijika kuona maendeleo haya chanya ya biashara katika kanda hii na ni matumaini yetu kuwa EAC itaendelea kuwa na ukuaji mzuri wa kibiashara na bidhaa zake zitaendelea kuleta ushindani mkubwa kutokana na ubora wake.

Tunatoa rai kwa nchi zote nane za EAC kuhakikisha zinaondoa vikwazo vyote vya kibiashara ambavyo vimekuwa vikileta usumbufu kibiashara ili mafanikio haya yasiishie hapa bali yawe mafanikio endelevu kwa afya ya uchumi wa kanda na nchi wanachama kwa ujumla.

Ni vema wakulima wa EAC kuhakikisha wanazalisha mazao bora yakayolikamata soko la kimataifa na hatimaye kuweza kushindana na mazao mengine ili mataifa yanayoagiza mazao ya EAC yasione sababu ya kuchukua mazao mengine kutoka kanda nyingine.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button