Hospitali ya Benjamin Mkapa kusogeza huduma

DODOMA : HOSPITALI ya Benjamin Mkapa ina mpango wa kuanzisha kliniki ya mjini lengo ni kusogeza huduma kwa wananchi katikati ya Jiji la Dodoma.
Akizungumza jijini Dodoma juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi amesema uamuzi huo wa kupeleka kliniki mjini kutawapunguzia adha wananchi ya kufuata huduma katika hospitali hiyo.
“Kama mnavyofahamu kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa iko kidogo pembeni ya mji, sasa tukiwa na ‘town clinic’ katikati ya mji tutawasogezea huduma mjini ili wananchi ambao hawahitaji kuja huku basi wapate huduma mjini,” alisema.
Aidha, Profesa Makubi amesema kwa sasa Hospitali ya Benjamin Mkapa ina huduma za kibingwa zipatazo 20 na huduma 17 ni huduma za ubingwa bobezi wa juu. “Kwa sasa wagonjwa wanaoonwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa imeongezea hadi wastani wa wagonjwa 1,200 kwa siku kutoka wagonjwa 900 kwa siku za nyuma, ongezeko hili limechangiwa na maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika.
Hivyo tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huu mkubwa na ambao umewezesha haya yote,” alisema. SOMA: Mavunde akabidhi magari mawili Hospitali ya Benjamini Mkapa
Amesema kwa mwaka 2024/2025, katika Hospitali ya Bejamin Mkapa imeshuhudia mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za afya kwa kuanzisha huduma mpya za ubingwa bobezi.
Hatahivyo, amezitaja huduma hizo kuwa ni upasuaji kwa njia ya matundu ya kuondoa figo mchangiaji kwenda kwa mgonjwa ambapo siku za nyuma upasuaji ulikuwa ukifanyika kwa kufungua tumbo ili kufikia figo.
Pia, wameweza kupandikiza uroto kwa mgonjwa akiwa wametofautiana makundi ya damu na mchangiaji, ikiwa ni tofauti na awali ambapo ilikuwa ni lazima makundi ya damu yafanane kati ya mchangiaji na anayewekewa uroto.
“Pia tumeweza kufanyia upasuaji wa ubongo, upasuaji wa mifumo ya mkojo, macho, moyo kwa kiwango cha kisasa kama ilivyo dira ya taasisi ya kutoa huduma za afya kwa kutumia teknolojia ya kisasa.Aliongezea kuwa, “mafanikio haya ndiyo yaliyoifanya Hospitali ya Benjamin Mkapa kuwa taasisi iliyotoa huduma bora za afya katika kundi la hospitali za ngazi ya kanda,” alisema.
Hivi karibuni, Hospitali ya Benjamin Mkapa imezindua huduma ya kliniki ya wagonjwa wa kimataifa na mashuhuri na huduma za uchunguzi wa afya wa kina. Profesa Makubi alisema kliniki hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 100 kwa siku na ina ubora wa kimataifa na wenye faida za ziada ikiwemo mgonjwa kutibiwa ndani ya muda mfupi.



