Mavunde akabidhi magari mawili Hospitali ya Benjamini Mkapa

DODOMA: MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde leo amekabidhi magari mawili ya wagonjwa kwa uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa yaliyotolewa na serikali ya India.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo katika viunga vya Hospitali ya Benjamin Mkapa huku yakishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospital ya Benjamin Mkapa Dk Alphonce Chandika.

Akizungumza katika hafla hiyo Mavunde amesema anaishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa magari hayo ya wagonjwa ambayo yatasaidia kuwahudumia wananchi.

Amesema, maboresho makubwa yamefanyika katika sekta ya afya jijini Dodoma ikiwemo ujenzi wa vituo vya Afya,Hospital ya wilaya na upatikanaji wa magari ya wagonjwa kwa vituo vya pembezoni na hivyo kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

“Nitajitahidi kwa nafasi yangu kuhakikisha tunaongeza gari jingine la wagonjwa kwa kuwa hospitali hii inahudumia watu wengi zaidi ya hospitali nyingi za hapa Dodoma hivyo ni muhimu kuboresha eneo hili,”Amesema Mavunde

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospital ya Benjamin Mkapa Dk Alphonce Chandika amesema magari hayo yatasaidia katika kusafirisha wagonjwa wa rufaa kutoka Hospitalini hapo na hivyo kutumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa magari hayo ya kisasa na yenye vifaa muhimu vya matibabu ambayo yatarahisisha utoaji huduma kwa wagonjwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa ya sekta ya afya mkoani Dodoma na kuutaka uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kuyatunza magari hayo na kuhakikisha yanafanya kazi iliyokusudiwa.

Habari Zifananazo

Back to top button