Rais wa MAT ataka mazingira ya uwekezaji yaboreshwe

DAR ES SALAAM: Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Mugisha Nkoronko, ametoa wito kwa Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya afya nchini.
Ameseme lengo kuiwezesha sekta binafsi kutoa mchango mpana na wenye tija katika utoaji wa huduma za matibabu kwa wananchi.
Dk. Nkoronko ameyasema hayo, wakati akiwasilisha mada katika Kongamano la Kitaifa la Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) lililojikita katika Sekta ya Afya.
Akichambua vikwazo vinavyoikabili sekta binafsi, Dk. Nkoronko aliangazia changamoto kubwa ya upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa, ambavyo mara nyingi huuzwa kwa gharama kubwa zinazoumiza mitaji ya wawekezaji wengi wa ndani.
Dk. Nkoronko amesisitiza kuwa uwekezaji wowote kwenye sekta ya afya hautakuwa na maana kama hautakwenda sambamba na uwekezaji mkubwa kwa wataalamu.
Pia ameikumbusha Serikali na wadau wa sekta binafsi kuongeza nguvu katika kuzalisha na kuwaendeleza wataalamu wenye ujuzi na uzoefu wa hali ya juu.



