Huduma kidijitali kufungua milango mapato ya nje

DAR ES SALAAM: WATANZANIA wanaojipatia kipato kupitia kazi za mtandaoni, ubunifu wa maudhui na biashara za kimataifa wanatarajiwa kunufaika na kurahisishwa kwa upatikanaji wa fedha wanazolipwa kutoka nje ya nchi, hatua inayoweza kuongeza fursa za kujiajiri na kuimarisha uchumi wa kaya.

Kupitia huduma mpya inayounganisha mfumo wa malipo wa PayPal na KCB Mobile App, Watanzania sasa wanaweza kuhamisha fedha kutoka akaunti zao za PayPal kwenda kwenye akaunti za benki, bila kutegemea baadhi ya njia za kati zilizokuwa zikitumiwa kupata malipo ya kimataifa.

Huduma hiyo iliyozinduliwa Oktoba 9, 2026, inafungua fursa kwa makundi mbalimbali yanayotegemea teknolojia kujipatia kipato, yakiwemo vijana wanaofanya kazi za kujitegemea, wabunifu wa maudhui, waandishi, wataalamu wa teknolojia na wafanyabiashara wa mtandaoni.

Kwa kundi hilo, upatikanaji wa njia rahisi za kupokea malipo kutoka nje unaweza kusaidia kupanua wigo wa wateja, kuongeza shughuli za kibiashara na kuwawezesha kufanya kazi katika masoko yanayovuka mipaka ya nchi.

Athari zake zinaweza pia kuonekana katika ngazi ya familia, ambako mapato yanayotokana na kazi za kidijitali yanaweza kusaidia kugharamia mahitaji ya kila siku, elimu, huduma za afya na shughuli nyingine za maendeleo.

Akizungumzia uzinduzi wa huduma hiyo, Mkuu wa Huduma za Kifedha za Kidijitali wa KCB, Josina Njambi, amesema ushirikiano huo unalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha za kidijitali kwa wateja wanaofanya kazi na wateja kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Huduma hiyo pia ni sehemu ya kampeni ya benki hiyo ya Ina-Make Cents, inayolenga kuhamasisha matumizi ya huduma za benki kupitia simu za mkononi.

Kuunganishwa kwa PayPal na KCB kunaongeza njia za kupokea mapato kutoka masoko ya kimataifa, kufuatia pia ushirikiano kati ya Vodacom M-Pesa na PayPal uliotangazwa Mei 2026.

Hata hivyo, pamoja na fursa hizo, gharama za miamala, viwango vya ubadilishaji wa fedha na masharti ya utoaji wa fedha ni mambo ambayo watumiaji wanapaswa kuyafahamu ili kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya huduma hizo.

Kwa ujumla, kurahisishwa kwa mifumo ya malipo ya kimataifa kunaweza kuwa sehemu ya kukuza uchumi wa kidijitali nchini, hasa kwa vijana wanaotumia ujuzi na teknolojia kujitengenezea ajira na vyanzo vipya vya mapato.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button