Huduma sekta ya madini kuanza kutolewa Mtumba leo

WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde amesema kuanzia leo huduma mbalimbali za Wizara ya Madini zitaanza kutolewa rasmi katika jengo la Makao Makuu ya Wizara hiyo lililopo eneo la Mtumba, Mji wa Serikali jijini Dodoma kutokana na kukamilika kwa mradi wa jengo hilo.
Amebainisha hayo wakati akizungumza na Menejimenti ya Wizara, taasisi zake pamoja na watumishi wa Wizara.
Waziri Mavunde ameishukuru Serikali kwa kuiwezesha Wizara kukamilisha jengo ambalo kwa sasa huduma zote zitatolewa hapo.
Amesema awali huduma zilikuwa zinapatikana sehemu tofauti tofauti kutokana na ofisi kuwa mbalimbali lakini sasa huduma zitatolewa sehemu moja na hivyo wadau kuondokana na usumbufu.
Awali, akiwakaribisha watumishi katika jengo jipya, Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa ameishukuru Serikali kwa kuweza kukamilisha ujenzi wa jengo na miundombinu mbalimbali itakayorahisisha utendajikazi na kutoa matokeo chanya kwa Sekta ya Madini kulingana na vipaumbele vyake.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amewapongeza watumishi wote wa Wizara kwa utendaji mzuri wa kazi katika mazingira yaliyokuwa yanawazunguka kwa kipindi chote cha ujenzi wa makao makuu, bila kujali changamoto zilikuwepo.
Aidha, kuhamia kwa Wizara katika Jengo jipya kunatimiza ahadi aliyoitoa Waziri Mavunde kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi Machi 20.
Jengo hilo la Wizara limejengwa na Mkandarasi Shirika la Nyumba la Taifa ( NHC) kwa gharama ya Shilingi bilioni 22.8 chini ya ushauri elekezi wa Wakala wa Majengo Tanzania ( TBA).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button