Hungary yapiga kura kujiondoa ICC

HUNGARY : BUNGE la Hungary limepiga kura kuunga mkono kujiondoa kwa nchi hiyo kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), hatua iliyochochewa na tuhuma za Waziri Mkuu Viktor Orbán kwamba mahakama hiyo inasukumwa na misukumo ya kisiasa.
Uamuzi huo wa Jumanne unamaanisha kuwa Hungary itajiondoa rasmi kutoka ICC ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, baada ya serikali ya Budapest kutoa taarifa rasmi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uamuzi huo.
Orbán alianza mchakato wa kujiondoa mapema mwezi Aprili, wakati wa ziara ya kitaifa ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, nchini Hungary. Uamuzi huu unafuatia uamuzi wa ICC kutoa hati ya kukamatwa dhidi ya Netanyahu na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant, kwa madai ya uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa na jeshi la Israel katika mzozo unaoendelea Gaza.
ICC pia ilitoa hati ya kukamatwa kwa kamanda mkuu wa Hamas, Mohammed Deif, ambaye inaaminika aliuawa na jeshi la Israel. Akizungumza April 3i, Orbán alisema“Tunaamini kuwa ICC imekuwa mahakama ya kisiasa. Miaka ya karibuni imeonesha kuwa hii si tena mahakama inayozingatia utawala wa sheria bali imepoteza usawa wake.”
Hungary ilisaini na kuridhia Mkataba wa Roma mwaka 2001 wakati wa muhula wa kwanza wa Orbán kama Waziri Mkuu, lakini haikuwahi kuuingiza rasmi katika sheria za kitaifa, ikidai kuwa mkataba huo unakinzana na katiba ya nchi.

Kupoteza Uadilifu na Uaminifu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Hungary, Péter Szijjártó, alisisitiza msimamo wa serikali dhidi ya ICC kupitia ujumbe aliouweka kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), akisema. “Kwa uamuzi huu, tunakataa kuwa sehemu ya taasisi ya kisiasa ambayo imepoteza uadilifu na uaminifu wake.”
Waziri wa Sheria wa Israel, Gideon Sa’ar, alipongeza uamuzi huo kupitia ujumbe wa pongezi kwa Hungary, akisema. “Asante Hungary kwa msimamo wenu wa maadili ulio wazi!”
Israel yenyewe imekuwa ikipinga mamlaka ya ICC juu ya raia wake na imeishutumu mahakama hiyo kwa kujaribu kuidhalilisha Israel kimataifa.
Mahakama ya ICC yachukua hatua ya kujitathmini
Wiki iliyopita, jopo la rufaa la ICC lilitoa agizo kwa mahakama ya chini kupitia upya pingamizi zilizowasilishwa na Israel kuhusu mamlaka ya ICC juu ya waranti za kukamatwa kwa Netanyahu na Gallant. Mahakama hiyo ya chini ilikuwa imekataa pingamizi hizo kwa msingi kuwa zilikuwa zimewasilishwa mapema sana, lakini jopo la rufaa lilisema hilo lilikuwa kosa la kisheria. Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa ICC imesema inatafakari uamuzi huo mpya kabla ya kutoa taarifa zaidi.



